Simba na Yanga, itumieni Mapinduzi Cup kimapinduzi.
Na Samuel Samuel
Nilikuwa VIP B tabasamu kubwa nikishuhudia wachezaji wa Yanga wakiichachafya Simba watakavyo. Katika lango la Dar young African alisimama kipa mwenye uwezo mkubwa wa kuipanga beki na kucheza krosi Ali Mustafa al maarufu kama Batezi.
Kipindi cha kwanza kilizidi kuing'arisha Yanga kwa kuongoza kwa mabao 3-0 huku mshambuliaji Mrisho Ngasa, akitimiza ahadi yake ya kuifunga Simba. Kabla ya mechi hiyo ya msimu wa 2013-14 Ngasa alitoa ahadi asipowafunga Simba atachoma moto nyumba zake zote tano anazomiliki.
Mpaka mapumziko Yanga ilikuwa mbele kwa magoli matatu. Kipindi cha pili kiligeuka na Batezi kujikuta akiokota mipira mara tatu ndani ya nyavu zake na mwisho matokeo yakasomeka 3-3.
Baada ya mechi hiyo sijamuona tena Batezi kukaa langoni kama golikipa wa Yanga. Ni mwaka sasa! Octoba 18 mwaka huu watani hawa wa jadi walikutana tena na timu ya Yanga ikipewa nafasi kubwa kushinda.
Achana na jinsi gani mechi hiyo ilichezwa lakini mkumbuke golikipa aliyesimama katika milingoti ya Simba SC. Manyika Jr aliwashitua wadau wa soka kwa uwezo mkubwa aliouonesha dhidi ya forward hatari za Yanga.
Kijana huyo wa miaka 18 alionesha kujiamini na uwezo mkubwa mbali na mechi hiyo pia alisimama vyema mechi na Mtibwa Sugar hata kuokoa penati iliyopigwa na David Luhende.
Wakati Yanga wana mgogoro na Juma Kaseja aliyesusia mazoezi basi wayatumie mashindano haya ya Mapinduzi kumrejesha mchezoni Ali Mustafa.
Dida apumzishwe ili kumnoa Batezi ili awe tayari kama golikipa namba mbili au hata ndani ya kikosi cha kwanza. Simba SC mnamuuguza Casilasi kwa sasa na goli la Atupele Green limewatoa imani juu ya Ivo Mapunda.
Ni muda wa kumjenga vyema Manyika Jr kama golikipa namba moja kwa michuano hii. Lazima tuwe na desturi ya kuwatumia na kuwaamini wachezaji. Utamlipaje mchezaji mshahara mwaka mzima bila hata kumpa dakika 10 uwanjani?
0 comments:
Post a Comment