Picha Msimbazi ndiyo kwanza linaanza.
Na Oscar Oscar Jr
Baada ya kuwasili Goran Kopunovic anayedaiwa kuwa kocha mpya wa wekundu wa Msimbazi klabu ya Simba, Mzambia Patrick Phiri amezungumza leo kuwa yeye bado ni kocha wa timu hiyo na hakuna kiongozi yoyote wa timu hiyo aliyompatia taarifa ya kusitisha mkataba wake.
Baada ya kuchezea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar kocha huyo aliingia kwenye sintofahamu na Uongozi wa timu hiyo ambao ulikuwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri kutokana na usajili wa gharama ambao wametoka kuufanya hivi karibuni.
Kesho kocha huyo anatarajia kusafiri kuelekea nyumbani kwao kwa matatizo ya kifamilia ambapo atakaa huko kwa muda wa siku mbili na kisha atarejea kuifuata timu hiyo ambayo imewasili leo huko visiwani Zanzibar kwa ajili ya michuano ya kombe la Mapinduzi.
Akizungumza kwa njia ya simu na mtangazaji wa kituo cha Redio cha E-FM, Phiri amesema kuwa bado yeye ni kocha wa Simba na kilichofanya asisafiri na timu kuelekea Zanzibar ni kutokana na matatizo yake binafsi ambapo ameomba ruhusa ya siku mbili kuelekea Zambia na kisha atarudi tena kuendelea na kibarua chake.
Kwa taarifa ambazo sio rasmi, Uongozi wa Simba umekuwa kimya na kushindwa kutoa tamko rasmi la kumtema kocha Phiri kutokana na kugawanyika. Lipo kundi la viongozi ambalo linapinga na lile ambalo linaunga mkono kocha huyo kutimuliwa.
Na kwa kitendo cha Phiri kuelekea Zambia huenda ndiyo amejipoteza moja kwa moja kwani kitakachofuata ni kupigiwa simu na kuelezwa namna atakavyolipwa stahiki zake.
0 comments:
Post a Comment