Searching...
Image and video hosting by TinyPic
31 December 2014
Wednesday, December 31, 2014

NIFIKIRIAVYO: TUUMALIZE MWAKA 2014 KWA SHUKRANI NA LAWAMA KATIKA SOKA.




Na Chikoti Cico

Leo ni tarehe 31 ya mwezi Desemba tarehe ya mwisho kabisa kwenye kalenda ya mwaka 2014 na haitokuja kujirudia tena hata kama jua likichomoza na kuzama mara ngapi, tarehe ya leo ikipita inamaanisha itakuwa ni tarehe nyingine na ya mwaka mwingine.

Na kwa mantiki hiyo naomba leo nitoe shukrani na lawama zangu kwa watu mbalimbali katika sekta ya mchezo wa soka dunia kote.

Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru mchezaji bora wa dunia mara mbili Christiano Ronaldo kwa kuendelea kuvunja rekodi mbalimbali za magoli ndani na nje ya klabu yake ya Real Madrid, sambamba na mpinzani wake mkubwa kwenye ufungaji Lionel Messi.

Hawa kwa mwaka 2014 waliendelea kutupa burudani ya pekee huku wakishindana kuzivunja rekodi za magoli ni aina ya wachezaji ambao ni waliubariki mwaka 2014.

Pili shukrani za dhati zimwendee Jurgen Klinsmann na Joachim Low, baada ya Ujerumani kunyakua kombe la Dunia nchini Brazili Joachim Low alimpigia simu Klinsmann kumpongeza na kumshukuru.

Hii ni kwasababu makocha hawa wawili ndiyo waliotengeneza programu ya timu ya taifa Ujerumani tokea mwaka 2004 na kuzaa matunda kwa kufanikiwa kunyakua kombe la Dunia mbele ya Brazili, Hispania, Argentina na Uholanzi.

Tatu Shukrani zangu ziwaendee Algeria ndiyo namaanisha timu ya taifa ya nchi ya Algeria iliyoko kaskazini mwa bara la Afrika kwa kucheza mpira na hata kuvuka hatua ya makundi ya kombe la Dunia kwa mwaka 2014.

Hii ndiyo kati ya timu ambayo haikuingia kwenye mkumbo wa timu za Afrika kuhangaikia posho kuliko kucheza mpira ni timu ambayo ilionyesha nidhamu na ari ya kulitetea bara la watu zaidi ya bilioni moja.

Shukrani za nne ziwaendee Azam na Mbeya City, niseme asanteni kwa kutuonyesha kwamba bila ya timu za Kariakoo bado ligi inaweza kupendeza kwa timu nyingine kuleta changamoto na hata kuchukua kombe, huku Mbeya City ikiingia kwa mara ya kwanza kwenye ligi kuu ya VODACOM na kushika nafasi ya tatu.

Shukrani za tano ziwaendee Mshambuliaji wa Azam Kipre Tchetche aliyeibuka mchezaji bora wa msimu uliopita wa ligi na aliyekuwa mshambuliaji wa Simba Amisi Tambwe aliyeibuka mfungaji bora wa ligi ya Tanzania bara kwa msimu uliopita kwa kufunga jumla ya magoli 19.

Hawa walionyesha thamani ya kwanini walisajiliwa kwa pesa nyingi na kwanini waliitwa wachezaji wa kigeni.

Kama msemo wa kiswahili unavyosema ukikubaliwa kusifiwa basi uwe tayari kulaumia basi nami naomba niwalaumu baadhi ya wadau kwenye mchezo wa soka duniani.

Nianze na shirikisho la soka nchini Tanzania yaani TFF hawa nawalaumu kwa kuchezea pesa za maendeleo ya soka letu nchini kwa kuanzisha kitu kilichoitwa maboresho ambacho hakikuleta tija yoyote kwa soka letu huku wajanja wachache wakijilia hela za bure bila kuboresha chochote na soka letu likiendelea kudidimia.

Pili nizilaumu timu niziite za "kujaribu makocha" yani timu kongwe kwenye fitna na kubadilisha makocha nikimaanisha timu za Simba na Yanga, ni mwaka mwingine kati ya mingi iliyopita ambapo timu hizi hazina jipya zaidi ya kuleta siasa kwenye soka na kubadili makocha kila mara.

Mpaka mwaka 2014 unafikia ukingoni tayari Simba na Yanga zimeshafukuza makocha wao ndani ya mechi nane tu toka kuanza kwa ligi kitu ambacho kinazidi kulifanya soka letu liendelee kudidimia na kukosa mwelekeo.

Ambaye ningependa pia kumlaumu pia ni Luis Suarez mshambuliaji wa Barcelona na timu ya taifa ya Uruguay hii ni baada ya kuitia aibu michuano ya kombe la Dunia iliyofanyika nchini Brazili kwa kumng'ata beki wa Italia Giorgio Chiellini.

kitendo hicho kilipelekea mchezaji huyo kufungiwa na shirikisho la soka Dunia lakini tayari Suarez alishaitia doa michuano hiyo mikubwa ya soka Duniani.

Mwingine aliyeutia aibu mchezo wa soka kwa.mwaka 2014 ni mchezaji wa Sheffield United Ched Evans aliyepatikana na hatia ya kumbaka binti wa miaka 19, huyu aliitia aibu timu yake lakini pia ligi daraja la kwanza nchini Uingereza na kiujumla aliutia aibu mchezo wa soka duniani kote kwa kitendo hicho kibaya na cha aibu.

Wakati timu ya Algeria ikijitahidi kuzifichia aibu timu za Afrika kwenye michuano ya kombe la Dunia Ghana, Kameruni, Nigeria na Ivory Coast hawa walilitia aibu bara la hili lenye watu zaidi ya bilioni moja kwa kupoteza muda mrefu wakihangaikia posho badala ya kucheza mpira.

Na tukio la ajabu kabisa ni kitendo cha wachezaji wa Ghana kushinikiza kutumiwa fedha nchini Brazili ili wakubali kucheza mchezo wa mwisho wa michuano hiyo dhidi ya Ureno kitendo kilichopelekea Raisi wa nchi hiyo kutuma ndege iliyobeba kiasi cha dola milioni 3 ili kuwapa wachezaji wa timu hiyo na ndipo walipokubali kucheza mchezo huo.

Najua kuna wengi ambao wanastahili kupongezwa na kulaumiwa pia lakini natumai hawa wachache wanaweza kutoa taswira ya vipi soka dunia kote lilivyokuwa kwa mwaka 2014 ambao utafikia tamati usiku wa saa 6 kamili wa tarehe 31 Desemba.

Mwisho niwatakie kila la kheri mashabiki wa soka dunia kote kwa 2015.
NAWASILISHA.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!