Searching...
Image and video hosting by TinyPic
28 November 2014
Friday, November 28, 2014

Uchambuzi: Sunderland vs Chelsea


Na Chikoti Cico

Ligi kuu nchini Uingereza inatarajiwa kuendelea leo kwa mechi kadha zitakazopigwa kwenye viwanja mbalimbali, kwenye uwanja wa Stadium of Light timu ya Sunderland itawakaribisha vinara wa ligi hiyo timu ya Chelsea katika kugombania alama tatu muhimu za mchezo huo.

Sunderland ambao walivunja rekodi ya kocha Jose Mourinho ya kutokufungwa kwenye uwanja wa Stamford Bridge katika mechi 78 kwenye msimu uliopita baada ya kushinda kwa magoli 2-1 wanatarajiwa kulenga kuvunja rekodi ya Chelsea ya kutokufungwa toka msimu huu uanze.

Kuelekea mchezo huo Sunderland watawakosa Emanuele Giaccherini, Billy Jones na Patrick van Aanholt ambao ni majeruhi huku Ricky Alvarez ambaye alikuwa majeruhi na kukaa nje kwa zaidi ya wiki sita akitarajiwa kucheza kwenye mchezo huo.

Kocha wa Sunderland Gus Poyet ambaye aliwahi kuichezea Chelsea kipindi cha nyuma anatarajia kuingia kwenye mchezo huo kutafuta ushindi wa tatu muhimu toka kuanza kwa ligi hiyo ili kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi ambapo mpaka sasa Sunderland inashika nafasi ya 14 ikiwa na alama 13.

Takwimu zinaonyesha Sunderland imepoteza michezo tisa iliyopita dhidi ya Chelsea kwenye uwanja wa Stadium of Light hivyo kama Chelsea atashinda mchezo wa leo basi itakuwa ni rekodi mpya kwenye ligi ya Uingereza kwa timu kupoteza michezo 10 mfululizo kwa wapinzani walewale.

Kikosi cha kocha Poyet kinaweza kuwa hivi: Pantilimon; Vergini, O'Shea, Brown, Reveillere; Cattermole, Larsson, Rodwell; Johnson, Wickham, Fletcher

Kwa upande wa Chelsea wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa hawana wachezaji wapya majeruhi zaidi ya Nathan Ake hivyo kocha Jose Mourinho anatarajiwa kufanya mabadiliko ya kikosi ili kuendana na ratiba ngumu ya kipindi cha mwezi Desemba mpaka Januari.

Huku wakiongoza kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 32 timu ya Chelsea itaingia kwenye mchezo huo kutaka kuendeleza rekodi ya kutofungwa toka kuanza kwa msimu huu wa ligi hivyo kuendelea kujikita zaidi kileleni.

Takwimu zinaonyesha kiungo wa Chelsea Cesc Fabregas ameifunga Sunderland magoli manne haya yakiwa ni magoli mengi zaidi kuliko timu nyingine yoyote huku pia akifunga magoli katika mechi tatu kati ya nne alizocheza na timu hiyo kwenye uwanja wa Stadium of Light.

Kikosi cha Kocha Mourinho kinaweza kuwa hivi: Courtois; Ivanovic, Terry, Cahill, Azpilicueta; Matic, Fabregas; Willian, Oscar, Hazard; Costa

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!