Searching...
Image and video hosting by TinyPic
13 November 2014
Thursday, November 13, 2014

Niyonzima huyooo!!


Na Oscar Oscar Jr

Kiungo wa kimataifa wa Rwanda na klabu ya Yanga, Haruna Niyonzima ametajwa na magazeti ya leo kutaka kuondoka kwenye klabu hiyo inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Niyonzimaa anatajwa kutoridhika na maisha ya wanajangwani hao kutokana na mfumo anaotumia kocha wa Yanga, Marcio Maximo na kitendo cha kiungo huyo mshambuliaji kutopewa nafasi ya kucheza kwa dakika zote 90. 

Tangu ujio wa Maximo, Niyonzima amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari akilalamikia kitendo cha kuchezeshwa dakika 45 za kwanza wakati yeye ana amini kuwa, bado ana uwezo wa kuitumikia timu hiyo kwa dakika zote 90.

Mchezaji huyo mwaka 2012 alihusishwa na kujiunga na wapinzani wa Yanga, timu ya Simba lakini dili hilo halikufanikiwa kutokana na maridhiano yaliyofikiwa baina yake na Uongozi wa Yanga na kukubali kusaini mkataba wa miaka miwili ambayo inamalizika mwishoni mwa msimu huu.

Kuna taarifa kuwa mchezaji huyo anataka kurudi kwao Rwanda na kujiunga na timu yake ya Zamani ya APR lakini, Simba pia wanatajwa kama watu wanaomfukuzia kwa karibu sana kiungo huyo.

Simba wanamsaka mchezaji wa kuimarisha safu yao ya kiungo ambayo inaweza kuwapoteza Amri Kiemba, Shabani Kisiga na Said Ndema kutokana na wachezaji hao kusimamishwa kwenye kikosi hicho cha Msimbazi kwa makosa mbalimbali.

Timu ya Simba kwa sasa, inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi kuu baada ya kujikusanyia alama tisa huku, Mtibwa Sugar wakiongoza ligi hiyo wakiwa na alama 15. 

Mechi za ligi kuu zimesimama kwa sasa kutokana na kupisha micheza ya kimataifa ya Kalenda ya Fifa.

Picha hii ni kwa mujibu wa website ya klabu ya Yanga.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!