Na Oscar Oscar Jr
Gareth Bale aliumia, akawa nje ya kikosi cha Real Madrid na kwa sasa amerejea. Unajua kinachotokea? analazimika kupigania namba yake mbele ya kiungo mwenzie, Isco. Bastian Schweinsteiger na Javi Martinez wameumia, Bayern Munich inazidi kuchanja mbuga kwenye Bundesliga na watakaporejea, watalazimika kupigania namba kwenye kikosi cha kwanza.
Ukiona shabiki wa Liverpool ana macho mekundu, usimfikirie vibaya. Mwenzio anaperuzi usiku na mchana kujua tarehe atakayorejea mshambuliaji, Daniel Sturridge. Wayne Rooney anapokosekana, Manchester United wanashika vichwa. Methieu Debuchy amekosekana, Arsenal wanalalamika utadhani wamemkosa Sergio Ramos!
Unajiuliza kwa nini klabu ya Manchester City haifanyi vizuri klabu bingwa Ulaya? usipate tabu, Manchester City ni timu ya kawaida tu. Manchester City sio timu bora kama watu wengi wanavyodhani.
Ni timu ya kawaida, inayotumia wachezaji wengi wa kawaida ambao imewanunua kwa bei kubwa na wanalipwa pesa ndefu!
Ukimuondoa David Silva, Sergio Aguero, Vincent Kompany na Yaya Toure, wengine ni wachezaji wa kawaida sana.
Ukienda Stoke City wapo, Southampton nako wapo na hata Sunderland utawakuta. Ukiambiwa utaje mabeki bora 20 barani Ulaya, sidhani kama utawajumuisha Martin Demichelis, Alexender Kolarov na Gael Clichy! Sidhani kama utafanya hivyo.
Anapokosekana Sergio Aguero, safu ya ushambuliaji inayumba. Maana yake Jovetic na Dzeko ni washambuliaji wa kawaida tu. Anapokosekana David Silva, safu ya kiungo mshambuliaji inayumba. Maana yake Nasri, Milner na Navas ni wachezaji wa kawaida. Sawa na anavyokosekana Yaya Toure, sawa na anavyokosekana Vincent Kompany mambo huwa hayaendi.
Ukitazama namna Manchester City alivyotwaa taji la ligi kuu Uingereza mara mbili ndani ya misimu mitatu ya hivi karibuni, unagundua kabisa kuwa, mapungufu ya vilabu vya Arsenal, Chelsea, Manchester United na Liverpool ni makubwa zaidi kuliko waliyonayo Man City lakini hilo halihalalishi wao kuwa timu bora Ulaya.
Ndugu yangu Chikoti Cico, ameandika makala hivi karibuni akibainisha sababu zinazofanya Manchester City wasitambe Ulaya. Ametaja umri mkubwa wa wachezaji, ametaji uchovu na nyingine kibao lakini, mimi bado naamini wachezaji wengi wa timu hiyo ni wa kawaida sana.
Kikosi cha Liverpool ambacho ndani kilijumuisha watu kama Javier Mscherano, Xaib Alonso, Steven Gerrard na Fernando Torres kilishindwa kupata ubingwa wa Uingereza. Manchester City ya leo kupitia watu kama Fernandinho na Joe Hart, wanaupata kiulaini tu!!
Ubingwa wa siku hizi wa Uingereza, hautokani na timu kuwa bora bali timu pinzani kuwa dhaifu zaidi. Siamini ubingwa wa 20 wa Manchester United kamaa ulitokana na timu hiyo kuwa bora, siamini mataji ya Manchester City mara mbili ndani ya miaka mitatu kama yanatokana na timu hiyo kuwa bora.
Bado naamini sababu kubwa ya timu ya Manchester City, kutofanikiwa kwenye klabu bingwa Ulaya ni kukosa wachezaji bora. Ukitazama orodha ya wachezaji 23 wanaowania Ballon D'or hapo mwezi Januari mwakani, Manchester City inawakilishwa na mchezaji moja tu, Yaya Toure.
Timu bora wachezaji wake wanapigania namba, timu bora haiyumbi kwa kumkosa mchezaji wake mmoja au wawili. Manchester City watu wanapiga pesa kuliko huduma wanayotoa. Wanapiga pesa kuliko viwango vyao. Klabu bingwa Ulaya, watasubiri sana.
0 comments:
Post a Comment