LEO dirisha la usajili Tanzania bara imefunguliwa rasmi na litafungwa tarehe 15 Desemba. Kocha mkuu wa Simba Mzambia, Patrick Phiri ameibuka na kusema kuwa, anahitaji kupata washambuliaji wawili huku akidai kuwa safu hiyo kwa sasa, haina uwezo mkubwa wa kufunga licha ya kutengenezewa nafasi nyingi.
Kikosi hicho cha Msimbazi kimefunga mabao saba katika mechi saba walizoshuka dimbani wastani wa bao moja kwenye kila mchezo kitu kinachoonekana kutomridhisha kocha wa timu hiyo. Mfungaji bora wa msimu uliopita, Amisi Tambwe amepoteza hali ya kujiamini huku akiwa na goli moja tu mpaka sasa.
Tambwe ameonekana sio chaguo namba moja kwa kocha Phiri na tayari amekuwa mtu anayetumia muda mwingi kusugua benchi. Uwepo wa mshambuliaji Elias Maguli na Mganda, Emmanuel Okwi kumemfanya Tambwe asiwe mfalme tena wa timu hiyo.
Kwa mujibu wa wekundu hao wa Msimbazi, Simba inajiandaa kuongeza washambuliaji wawili na kwa hali hiyo, Amis Tambwe hatokuwa na jipya tena.
Pamoja na wachezaji wengi kama Haruna Niyonzima, Juma Kasseja, Simon Msuva kutajwa kuwindwa na timu ya Simba, kocha huyo amekiri pia kuwa kitendo cha kuwakosa Haruna Chanongo na Amri Kiemba ni pigo kwenye kikosi chake.
Wachezaji hao walisimamishwa na Uongozi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni hujuma kwa timu hiyo. Wachezaji hao wanadaiwa kucheza vizuri zaidi wanapokuwa na timu ya Taifa kuliko vile wanavyocheza wakiwa na klabu yao.
Simba kwa sasa wanakamata nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi kuu na wanatarajia kushuka dimbani tena tarehe 26 Desemba kuwakalibisha Kagera Sugar kutoka mkoa wa Kagera mchezo utakaopigwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kagera Sugar kwa sasa wapo kwenye nafasi ya tano huku wakiwa na pointi 10.
0 comments:
Post a Comment