Searching...
Image and video hosting by TinyPic
15 October 2014
Wednesday, October 15, 2014

UCHAMBUZI: Mbeya City vs Azam fc Jumamosi hii.


Na Oscar Oscar Jr

Mwishoni mwa juma hili pale Mbeya katika dimba la Sokoine, kutakuwa na mpambano baina ya Mbeya City dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi kuu bara timu ya Azam. 

Tayari kwa sasa Mbeya City wanaona wameshafikia uwezo wa Azam ndani ya dakika 90 za kipute uwanjani pamoja na kuwa timu hizo zina tofauti kubwa sana kiuchumi.

Mpaka sasa Mbeya City ndiyo timu pekee kwenye ligi kuu ambayo haijaruhusu kufungwa hata goli moja kwenye michezo mitatu ya awali ingawa, safu yao ya ushambuliaji haionekani kuwa na makali kwani wamefunga mpaka sasa bao moja tu. 

Azam wanashika nafasi ya pili baada ya kujikusanyia alama saba kwenye michezo mitatu nyuma ya Mtibwa Sugar wenye alama tisa huku Mbeya City, wakiwa kwenye nafasi ya nne baada ya kuambulia alama tano. Azam wameshafunga mabao matano na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara moja.

Mchezaji wa kuchungwa kwa Mbeya City.

Mwagane Yeya ni mshambuliaji ambaye pamoja na kuwa hajafunga goli lolote hadi sasa, uwezo wake na historia dhidi ya timu ya Azam, vinanifanya niamini kuwa ana uwezo wa kuifunga timu hiyo. 

Msimu uliopita alifunga mabao matatu dhidi ya Azam pale Azam Complex na mchezo wa marejeano pale Sokoine, pamoja na kuwa Mbeya City walipoteza mchezo kwa kufungwa bao 2-1, yeye ndiye aliyekuwa mfungaji wa bao hilo pekee.

Mchezaji wa kuchungwa kwa Azam fc.

Didier Kavumbagu ndiye anayeongoza kwa kupachika mabao kwenye ligi kuu bara mpaka sasa akiwa na magoli manne katika michezo mitatu. Ni aina ya mshambuliaji aliyekamilika, anajua kulazimisha nafasi za kufunga na anapopata nafasi huwa hafanyi makosa. Katika misimu yake miwili ya ligi kuu bara, amefunga zaidi ya magoli 20.

Mechi tatu za Mbeya City za hivi karibuni.

Mbeya City 0-0 JKT Ruvu
Mbeya City 1-0 Coastal Union
Ruvu Shooting 0-0 Mbeya City

Mechi tatu za Azam za hivi karibuni.

Azam 3-1 Polis Moro
Azam 2-0 Ruvu Shooting
Tanzania Prisons 0-0 Azam

Pamoja na kuwa Azam ilimaliza msimu uliopita ikifungwa magoli machache kuliko timu yoyote (15), mpaka sasa wameendelea kujilinda vema na wameruhusu bao moja pekee. 

Siku ya jumamosi  watakuwa na kazi ya ziada pale watakapo kutana na washambuliaji wenye njaa ya magoli kama Themi Felix, Paul Nonga na Mwagane Yeya kule jijini Mbeya. 

Mchezaji bora wa ligi kuu na mfungaji bora wa klabu ya Azam wa msimu uliopita, Kipre Tchetche bado hajafunga goli hata moja lakini uwezo anaouonyesha dimbani, sio mtu wa kumbeza hata kidogo. Golikipa wa Mbeya City, Davidi Burhan atalazimika kujiandaa kuzuia mashuti makali ya kijana huyo wa wanalamba lamba.

Agrey Moris na Said Morad, wanatakiwa kuwa kwenye kiwango cha juu kuelekea mchezo huo. Azam ndiyo time pekee ambayo imewahi kuondoka na alama zote tatu dhidi ya Mbeya City kwenye dimba la Sokoine, walifanya hivyo msimu uliopita. Je, wanauwezo wa kufanya hivyo tena? pengine hiki ndicho kinachosubiriwa na wengi.


















uwanuwanjani

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!