Hivi Nauli ya Zurich na mshahara wa Mwanasheria wa Yanga havina kazi nyingine?
Na Chicoti (Cico cicod)
0755 700 076
Kuna wakati nawaza hivi tumelogwa au tumelelewa vibaya, ama tumeachiwa laana ila ni ngumu kupata jibu la haraka haraka hasa katika nchi ambayo rasilimali ni nyingi lakini bado inaitwa ni nchi maskini.
Nchi ambayo ajali ya gari inaua watu 40 lakini hakuna mtu anashtuka kwasababu tu waliokufa ni makabwela wasio na sauti hivyo hakuna hatua zozote zitachukuliwa kuepuka ajali nyingine kesho.
Hii ndiyo nchi ambayo maamuzi ya msingi yana amuliwa kwa kura ya ndiyo na hapana huku hoja za msingi zikibaki kwenye makaratasi kama sehemu tu ya hadidu rejea ama kwa kiingereza “reference” ukiuliza kwanini utajibiwa “we utakuwa umetumwa”.
Umesikia siasa ya sakata la Yanga dhidi ya Okwi, baada ya maamuzi kufikiwa na TFF kupitia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji juu ya kumuweka huru Okwi na kumhalalisha kuichezea Simba.
Yanga wameamka na sasa siasa imechukua nafasi yake huku viongozi wa Yanga wakisisitiza kwamba uamuzi huo ni batili na wanataka kwenda kukata rufaa FIFA/CAS.
Pamoja na sababu nyingine ila taarifa zinasema mkataba wa Okwi na Yanga ulivunjwa pale tu Yanga waliposhindwa kumlipa Okwi awamu ya pili ya stahili zake kama mkataba ulivyokuwa unasema, hivyo toka tarehe 27 Januari 2014 Okwi alikuwa mchezaji huru, sasa unajiuliza hizo habari za kwenda kukata rufaa FIFA zinatoka wapi?
Na hapa ndipo unapoona jinsi viongozi wa Yanga wanavyoleta siasa, unaposhindwa kumlipa mchezaji stahiki zake kama ambavyo mkataba ulisema ni wazi kwamba hapo mkataba umekiukwa.
Nawaza hivi Mwanasheria wa Yanga hakuliona hili mapema toka Januari 27, 2014? Na kama hakuliona basi mshahara anaolipwa na Yanga ni bora utumike kwa kazi nyingine.
Ukiachana na mshahara wa Mwanasheria wa Yanga kuna hili la kwenda kukata rufaa Zurich, Uswisi yalipo makao makuu ya FIFA, hapa tena unajiuliza kwa kipengele kile kile cha kushindwa kumlipa stahili zake Okwi kama mkataba ulivyosema, Yanga wanapata wapi ujasiri wa kwenda kukata rufaa FIFA?
Nafikiri ni vyema hiyo nauli ya kwenda Zurich ikatumika kwa shughuli nyingine za klabu na viongozi wa Yanga kuachana kabisa na swala la Okwi hasa ukizingatia tayari kocha Marcio Maximo ashaanza programu yake ambayo haimuhusishi Emmanuel Okwi.
Ila usishangae sana kwa siasa za viongozi wa Yanga katika swala la Okwi kwasababu kiongozi wa jumuiya ya kisovieti kwenye miaka ya 1950 Nikita Khrushchev aliwahi kusema “Wanasiasa wako sawa kila mahali, wataahidi kujenga daraja hata mahali ambapo hakuna mto”
0 comments:
Post a Comment