Luiz Nani nje, Marcos Rojo ndani ya Old Trafford
Na Oscar Oscar Jr
Baada ya kuchezea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa timu ya Swansea wakati wa ufunguzi wa pazia la ligi kuu, Manchester United ilionyesha udhaifu mkubwa sana hasa kwenye safu yake ya ulinzi.
Man United iliwapoteza mabeki wake mahiri Nemanja Vidic, Patrice Evra na Rio Ferdinand baada ya msimu wa 2013/2014 kumalizika na hivyo wanahitaji mbadala wa walinzi hao walioitumikia klabu hiyo ya Old Trafford kwa mafanikio.
Sporting Lisbon wamekubali kuwauzia Manchester United beki wa kushoto Marcos Rojo aliyechezea Argentina Kombe la Dunia huku Nani akijiunga nao kutoka klabu hiyo ya Ligi ya Premia kwa mkopo.
Sporting walisema kupitia taarifa kwa Tume ya Soko la Hisa la Ureno kwamba klabu hiyo ya Ligi ya Premia italipa €20 milioni kumchukua mchezaji huyo wa miaka 24 lakini klabu hiyo ya Ureno haitalipa chochote kumchukua Nani kwa mkopo wa mwaka mmoja.
Rojo alifana sana kwenye Kombe la Dunia, akiwa kwenye safu ya ulinzi ya Argentina iliyofungwa mabao manne pekee katika mechi saba na wakamaliza wa pili nyuma ya Ujerumani.
Ujio wa beki huyo huenda ukafungua milango kwa wachezaji wengine wanaohitajika Old Trafford hasa kiungo mkabaji na beki wa kati mwenye uwezo mkubwa.
0 comments:
Post a Comment