Searching...
Image and video hosting by TinyPic
2 August 2014
Saturday, August 02, 2014

Karibu Elias Maguli Msimbazi



Na Oscar Oscar Jr

Elias Maguli amejiunga na klabu ya Simba akitokea klabu ya Ruvu Shooting ambako msimu uliopita, alikuwa mfungaji bora kwenye klabu yake baada ya kutimiza mabao 13 ya ligi. 

Simba walimuhitaji Maguli? pengine hili linaweza kuwa miongoni mwa maswali rahisi kabisa kujibu kwa sababu hata kama hujawahi kumuona uwanjani unapoangalia tu idadi ya mabao yake, utasema ndiyo.

Ukitazama washambuliaji wa Simba msimu uliopita, utakutakana na Amis Tambwe aliyefunga mabao 19, Haruna Chanongo akifunga mabao matano na Bertram Mombeki akishika nafasi ya tatu kwenye klabu akiwa na mabao manne tu. Unaanzia wapi kumkataa Maguli? labda kama unalako jambo lakini je, anaiweza Simba?

Unapocheza klabu ya Simba ni tofauti kabisa na unapokuwa Ruvu Shooting, Simba kuna presha kubwa kuliko Ruvu, Mashabiki na viongozi sio wavumilivu sana kama wa Ruvu na ndiyo maana haishangazi kuona kocha King Kibadeni aliyefikisha alama 24 mzunguko wa kwanza akitimuliwa huku Zdravko Logarusic aliyefikisha alama 14 kwenye michezo 13 ya mzunguko wa pili akibakizwa klabuni.

Malengo pia ya Simba ni tofauti na yale ya Ruvu Shooting na ndiyo maana wachezaji wengi sana wanachemka. Kukosa nafasi moja ya wazi ya kufunga, inakuwa nomgwa kwa mshambuliaji. 

Simba wanahitaji kushinda ubingwa wa ligi kuu ambao wameukosa kwa miaka kadhaa sasa hivyo ni lazima Maguli ajue namna ya kutuliza presha.

Elias atalazimika kupigania namba pia kitu ambacho kisingeweza kutokea endapo angebakia Ruvu kwa sababu kule alikuwa Star wa timu tofauti na itakavyokuwa Simba. 

Tayari Paul Kiongera raia wa Kenya na Jerome Rama wa Botswana wanatajwa kuja Simba huku mtu mzima Tambwe yeye akiwa na uhakika wa namba je, Maguli yuko tayari kupigania namba? pengine muda ndo utaamua.

Bado naamini Elias Maguli ni aina ya mchezaji mwenye uwezo wa kung'aa ndani ya msimbazi kama ataamua kujituma na kuonyesha ubora wake. 

Kujiunga na Simba sio jambo rahisi lakini kupotea ukiwa hapo ni jambo la muda mfupi sana. Sifa kubwa ya mshambuliaji bora ni kufunga mabao, kusaidia kukaba na majukumu mengine ni nyongeza tu. Karibu sana Maguli mtaa ya Msimbazi.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!