Na Oscar Oscar Jr
oscargeorge55@yahoo.com
Kuna wakati huwa tunapenda kulazimisha mambo kabla ya wakati wake.Ni jambo la kawaida kabisa kumuona binti anayesoma kidato cha pili akitamani kushika ujauzito na yeye apate mtoto! Anasahau kabisa kwamba kuna muda utafika,atazaa watoto mpaka achoke. Umeanza kufanya kazi leo,kesho tayari unataka uwe na nyumba yako na usafiri wa maana! unadhani ni rahisi kiivyo eeh? unahitaji kuwa na malengo,jitihada na subira ya hali ya juu ili kuweza kufanikiwa maishani.
Christiano Ronaldo ni moja kati ya wachezaji waliopitia mambo mengi sana ya kukatisha tamaa lakini siku zote ameendelea kujituma,ameendelea kufanya kazi yake kwa kiwango bora kabisa na kupuuza wale wote waliokuwa wanambeza.Ronaldo amekuwa kwenye ubora kwa muda mrefu sana na sasa nadhani ndiyo muda wake wa kurudisha yale "magoli" yote ya Ballon D'or aliyofungwa na Lionel Messi.
Mwezi Januari mwaka huu wakati Ronaldo anatangazwa kuwa mchezaji bora wa dunia huku akiwabwaga wapinzani wake Lionel Messi kutoka Barcelona na Frank Ribery wa Bayern Munich,tukio hilo lilionekana kutomfurahisha Ribery ambaye alikuwa ametoka kushinda mataji matatu.Unajua kwa nini Ribery hakuridhika? pengine alikuwa anajua fika kuwa hana uwezo wa kurudia mafanikio aliyopata mwaka jana na ndiyo maana,alitaka wamalizane pale pale.Unadhani atapata hata nafasi ya tatu tena? binafsi hata kwenye 23 bora,sioni jina lake.
Wapinzani wa Ronaldo kwenye Ballon D'or mwaka jana,wote wanapumulia mitambo kwa sasa.Frank Ribery sio yule tena,siku hizi anakamatika tu kirahisi,hana makeke,hana jipya.Lionel Messi amechoka,sio yule tena.Namba ya jezi ya messi imekuwa kubwa kuliko magoli aliyofunga msimu huu kwenye klabu bingwa Ulaya!
Frank Ribery amekuwa mchezaji anayelalamika zaidi kwa waamuzi kuliko mashuti yake yanayolenga goli! Unakumbuka bwana mdogo Daniel Carjaval wa Real Madrid alivyomshika mtu mzima kwenye mechi zao mbili za klabu bingwa Ulaya? Unadhani ingekuwa rahisi kwa dogo huyo kumzuia Ribery misimu miwili ya nyuma? hapana,Ribery ameanza kupotea uwe unapenda au hupendi.
Pamoja na heshima kubwa ninayompa Lionel Messi lakini,huyu Messi wa leo sio yule aliyeshinda Ballon d'or mara nne mfululizo.Majeruhi ya mara kwa mara na kushuka kiwango kwa timu nzima ya Barcelona,pengine ni moja ya sababu zinazomfanya mshambuliaji huyo hatari kusoma "Plate number" za Ronaldo msimu huu.
Ukitaka kuanzisha mjadala wa soka ambao hautakuwa na mwisho,basi weka mada inayomgusa Ronaldo na Messi.Kirahisi tu,mtu anaweza kukuambia kuwa Messi ni kipaji asilia na Ronaldo ni ubora unaotokana na mazoezi! Kirahisi tu,mtu atakuambia kuwa Messi ni mpole na hana majivuno kama ilivyo kwa Ronaldo! Unadhani kwa vigezo hivyo ni lini watu hao watamaliza ubishi? hakuna siku watakayokubaliana.
Hata Rais wa FIFA mwenyewe Sepp Bratter, hili jambo limemshinda.Kauli zake juu ya ubora wa wachezaji hawa,hazina tofauti na zile za rafiki zangu ambao kila mwishoni mwa juma huwa tunakutana kuangalia mechi kwenye vibanda umiza.Juzi wakati Christiano Ronaldo anaisambaratisha timu ya Bayern Munich pale Allienz Arena,nadhani Rais wa FIFA alikuwa amejificha chini ya meza.
Inawezekanaje watu ambao wanadhaniwa kuwa kwenye ubora unaokaribiana kwenye kila kitu,halafu mmoja awe na tuzo nne za Ballon d'or mfululizo na mwingine msindikizaji kila siku? maswali kama haya yangeulizwa misimu mitatu ya nyuma,ingekuwa vigumu sana kupata majibu lakini usipokata tamaa na kuendelea kupambana,kuna muda hata kuchakachua inashindikana.
Ronaldo kwa sasa anaongoza kwa magoli kwenye ligi ya mabingwa Ulaya huku akiwa na mabao 16 ambayo ni mara mbili ya mabao 8 yaliyofungwa na Lionel Messi na mara tano na cheji inabaki mbele ya Ribery mwenye mabao 3 tu.Hivi unamjua Ronaldo au unamsikia? mabao yake mawili aliyofunga kwenye ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Bayern,yalimfanya avunje rekodi ya Messi ya kufunga mabao 14 ya UCL kwenye msimu mmoja na sasa,Ronaldo ameweka rekodi nyingine ya kufikisha mabao 16.Bado una swali tu?
Kama Ronaldo atafanikiwa kuisaidia timu yeke ya taifa ya Ureno kwenye michuano ya kombe la dunia inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwaka huu mwezi juni kwa angalau kutinga hatua ya nusu fainali,bila shaka kitakachokuwa kinasubiriwa ni busu tu maridadi la mwanadada Irina Shayk ambaye ni mpenzi wake pale shujaa huyo atakapokuwa anachukuwa tena Ballon D'or mwakani.Unadhani hii tuzo itakwenda kwingine? hapana,itarudi tena kwa Ronaldo.
naomba kutoa hoja.
0 comments:
Post a Comment