COASTAL UNION KIMENUKA SASA
NA HAFIDH KIDO
MIMI Hafidh Athumani Kido, nikiwa na akili timamu natangaza kutojihusisha na shughuli zote za Coastal Union, hasa usemaji wa klabu.
Miongoni mwa sababu nyingi zilizonifanya kutangaza uamuzi huo ni sintofahamu iliyozuka ndani ya klabu yetu, kwa taaluma yangu ya uandishi wa habari lazima niwe na msimamo juu ya mambo yanayoendelea kwenye jamii.
Ili niendelee kufanya kazi na klabu hii kwa wakati huu wa misuguano, lazima niwe na upande; kwa maana upande unaounga mkono uongozi ama upande usiokuwa na Imani na uongozi. Lakini mimi nimeamua kutounga mkono upande wowote.
Kwa hivyo basi, ili niwe katika mstari sahihi nimeamua kukaa pembeni nifanye shughuli zangu za uanahabari kwa furaha na amani.
Kwa kipindi kirefu nimekuwa nikijaribu kuzima habari za uzushi na kuisimamia klabu isiyumbishwe na mijadala ya hovyo, lakini kutokana na kuwa mbali na klabu, na ama kutopewa taarifa sahihi hata ninapoziuliza kwa viongozi; nimeona si wakati salama wa kukuza uwezo wangu wa kiusemaji hasa ikizingatiwa bado ni kijana na sihitaji kuharibu hadhi yangu.
Bado ni mwanachama halali wa Coastal Union Sports Club, namba yangu ya kadi ni 0013. Nitaendelea kutoa ushauri na kuishabikia klabu yangu ambayo nimekuwa nikimuona marehemu baba yangu na kaka zangu wakiishabikia tangu nikiwa mdogo.
Kadhia kubwa ni kuhusu uhalali wa Nassor Ahmed Binslum, kuwa ni mfadhili ama mtu tu aliekuwa akiinyonya klabu yetu kupitia kampuni yake ya matairi na betrii (Binslum Tyres Company Limited).
Kwa hilo nasema wazi bila kupepesa macho, kuwa Nassor Binslum ndie alienishawishi kuwa msemaji wa klabu baada ya aliekuwa msemaji Edo Kumwembe, kujiengua kutokana na sababu za kutingwa na majukumu ya kiuandishi.
Binslum, huyohuyo ndie aliefanikisha kununua kamera inayotumika kuendesha shughuli za klabu, ndie alieninunulia kompyuta mpakato (Laptop), ninayoitumia kwa shughuli za klabu, mtu mmoja huyohuyo ndie aliekuwa akinifadhili katika safari za klabu kama pesa za nauli na chakula.
Binslum huyohuyo, ndie aliefadhili kuanzishwa kwa blogu ya klabu ambayo amekuwa akiifuatilia kila siku na hata marekebisho madogomadoo yeye ndie anaeyasimamia kwa kutoa fedha.
Binslum huyohuyo aliekuwa hafai ndie alieshinikiza niwemo kwenye ziara ya Oman, timu ilipoweka kambi kwa wiki mbili. Kwani viongozi walio madarakani hawakuona umuhimu wangu wakaamua kukata jina langu mpaka siku moja kabla ya pasi za kusafiria kupelekwa ubalozini.
Binslum, alinipigia simu saa kumi alasiri akinitaka kupeleka pasi yangu ya kusafiria kwa meneja wa timu ambae hakutaka kupokea simu yangu kila nilipompigia, na hata nilipompigia mwenyekiti wa klabu akaahidi atawasiliana na meneja wa timu lakini mpaka jua linazama hakukuwa na msaada wowote niliopewa, nikaamua kufanya kitendo cha hatari kwa kuenda kuiwacha pasi yangu ya kusafiria kwa muhudumu wa hoteli aliyofikia meneja hapa jijini.
Lakini hata alipoipata asubuhi yake pia hakuniarifu kuwa ameipata yaani mpaka siku ya safari sikuwa na uhakika kama nilikuwa miongoni mwa wasafiri ama la. Kwa kifupi nilikuwa nikichezwa shere.
Kwa hivyo basi ikiwa Binslum, hatakiwi na klabu nitakuwa mnafiki kuendelea kubaki kwasababu nitakuwa sawa na mnyama ninaetia ulimi puani.
Mtashangaa nimetangaza uamuzi huu wa kuachia ngazi bila kusema kuwa nimeandika barua ama la, kifupi sina mkataba wala taarifa yoyote ya kimaandishi juu ya kuajiriwa kwangu na klabu. Hivyo nimeamua kujiuzulu kienyeji kama nilivyoitwa kienyeji.
DAR ES SALAAM, TANZANIA
0713 593894
0 comments:
Post a Comment