TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Na Ezekiel Kamwaga.
UONGOZI wa Simba SC unapenda kuwashukuru wanachama na washabiki wake wote hapa nchini kutokana na mshikamano mkubwa waliounyesha wakati wa kuelekea kumalizika kwa Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu.
Ingawa matokeo hayakuwa mazuri siku zote, lakini mapenzi ambayo washabiki walionyesha kwa klabu yao lilikuwa ni jambo la faraja kwa uongozi, benchi la ufundi pamoja na wachezaji.
Wachezaji wa Simba pia wameelezea kufurahishwa kwao na namna washabiki waliokwenda kwenye Uwanja wa Taifa kutazama pambano la Watani wa Jadi Jumamosi iliyopita, walivyowashangilia kwa dakika zote tisini.
Uongozi wa Simba unapenda kuwaahidi washabiki wake kwamba utafanya kila uwezalo kuhakikisha kwamba klabu inajiandaa vya kutosha kufanya vizuri msimu ujao.
Makosa ambayo yalisababisha timu isifanye vizuri msimu uliomazika yatatazamwa na kufanyiwa upembuzi yakinifu ili yasijirudie tena katika msimu unaokuja na mingine.
Simba SC inaamini kwamba wanachama wake watakuwa bega kwa bega na uongozi kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri msimu ujao.
MAPATO
Msimu huu ulikuwa na changamoto kubwa sana za kimapato. Katika mechi baina ya Simba SC na Ashanti iliyochezwa jijini Dar es Salaam, mgawo kwa Simba SC ulikua ni zaidi kidogo ya shilingi laki tatu. Hii ni rekodi katika historia ya Simba.
Hili lilisababishwa zaidi na kutofanya vizuri kwa timu. Hata hivyo, uongozi ulijitahidi kwa kadri ilivyowezekana kupambana na changamoto hizi kwa kutumia vyanzo vyake vya ndani na ubunifu.
Pamoja na changamoto zote hizo, uongozi ulijitahidi kuisimamia timu na hata katika mechi ya Watani wa Jadi iliyofanyika Jumamosi iliyopita, timu iligharamiwa na viongozi waliopo pasipo kupata msaada wowote kutoka nje ya uongozi.
Kupitia uzoefu uliopatikana msimu huu kwenye eneo la mapato, uongozi sasa utabuni namna nyingine za kuongeza mapato ili kupambana na changamoto za kupungua kwa mapato ya milangoni.
TIMU
Mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu, klabu imevunja kambi na wachezaji wote wamepewa ruhusa ya kupumzika hadi katika wiki ya kwanza ya mwezi Julai mwaka huu ambapo timu itaanza mazoezi kujiandaa na msimu ujao.
Na kama ilivyo katika vitabu vya Sayansi ya Michezo, Simba itafanya mazoezi ( Pre Season) kwa walau wiki sita kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu msimu ujao. Simba haitakuwa na mechi yoyote ya kirafiki na wala haitashiriki mashindano yoyote yatakayokuwa yameandaliwa katika kipindi cha kati ya mwezi Juni au Julai; labda kama benchi la ufundi litaona inafaa.
KOCHA LOGARUSIC
Uongozi wa Simba unaendelea na mazungumzo na kocha wake, Zdravko Logarusic, kuhusu kumuongezea mkataba wake na mazungumzo hayo yatafikia tamati mwishoni mwa wiki hii.
Klabu itatoa tamko rasmi kuhusu endapo itaendelea au haitaendelea na mkataba wake na kocha huyo baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo. Kwa sasa, haitazungumzia lolote kuhusu hilo hadi mwishoni mwa wiki hii.
Imetolewa na
Katibu Mkuu
Simba SC
0 comments:
Post a Comment