Na Oscar Oscar Jr
Bayern Munich hawatawapa idhini wanahabari wa magazeti mawili ya udaku ya Uingereza The Sun na Daily Mirror kuhudhuria mechi ya marudiano ya robofainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Manchester United kutokana na kile washindi hao wa mataji matatu msimu uliopita walisema ni kuandikwa kwa ripoti za kuchukiza baada ya sare ya 1-1 wiki hii.
Bayern watakuwa wenyeji wa United wiki ijayo na Wajerumani hao wanapigiwa upatu kusonga mbele licha ya kuwa watakosa kiungo wao wa kati Bastian Schweinsteiger baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu wakiwa Old Trafford.
"Baada ya mechi ya kwanza, magazeti hayo mawili ya Uingereza yaliripoti kuhusu mchezaji wetu Bastian Schweinsteiger kwa njia ya kuchukiza naya kumtusi,” Bayern walisema kupitia taarifa Alhamisi.
"Bayern Munich haikubali uanahabari wa aina hii na inakashifu sana vitendo hivyo.”
Magazeti hayo mawili yalikuwa yameandika vichwa vya habari sawa baada ya kufukuzwa kwa Schweinsteiger dakika za mwisho kwa kumchezea vibaya Wayne Rooney wakitumia jina la Kijerumani la nguruwe ambalo ni 'Schwein'.
"You dirty Schwein," (Wewe nguruwe mchafu), kilisema kichwa cha habari cha Mirror kilichoambatana na picha ya Schweinsteiger. Kichwa cha habari cha The Sun kilisoma "You Schwein." (Wewe Nguruwe).
Vichwa hivyo vya habari vilizua shutuma kali Ujerumani wiki hii.
"Bayern Munich hawatawapa ruhusa wawakilishi wa Daily Mirror na The Sun kuhudhuria mechi ya marudiano Aprili 9,” walisema Bayern.
0 comments:
Post a Comment