KOCHA ROBERTO MARTINEZ AONYESHA HESHIMA KWA ARSENAL
Meneja wa Everton, Roberto Martinez, amekaribisha changamoto ya kumaliza miongoni mwa nne bora katika ligi ya Premier ya Uingereza baada ya timu yake kuwabwaga wenyeji Fulham 3-1 Jumapili katika uwanja wa Craven Cottage.
Huo ulikuwa ushindi wao wa tano wa hivi karibuni na kufunga mwanya kati yao na Arsenal walioko nafasi ya nne hadi pointi nne huku wawili hao watamenyana wikendi hii wakati Everton watakapowaalika Gunners nyumbani kwao Goodison Park.
Arsenal wamepoza moto baada ya kupata alama tano pekee kati ya 15 walizowania na kupelekea mwalimu wao Arsene Wenger kuzungumzia haja ya kutizama wanao wafuata kwenye harakati za kufuzu kombe la mabingwa kwa kumaliza miongoni mwa nne-bora.
“Changamoto tuliyonayo sasa ni Jumapili dhidi ya Arsenal. Ingawa tunawaheshimu, kukiri kwao kuwa wanatizama begani wanaowafuata ni kithibitisho kuwa tumekuwa na msimu bora kwani wenzetu,wamefuzu kombe la mabingwa kwa miaka 18 au 19 iliyopita mfululizo.
“Wanaelewa jinsi ya kuwania hadhi hii kipindi hiki cha msimu lakini tuna nafasi bora ya kupigania azimio hilo,” Martinez alinena.
Baada ya kudorora katika kipindi cha kwanza Everton waliinuliwa na mabadiliko yaliowaleta Steven Naismith, Kevin Mirallas na Aiden McGeady kutoka benchi.
Walitwaa uongozi kupitia bao la kujifunga wenyewe la kipa wa Fulham, David Stockdale lakini Ashkan Dejagah aliposawazisha na kombora maridadi.
Mirallas na Naismith waliongeza mabao mawili mechi hiyo ikikaribia kwisha kunoa makali yao kabla ya kuwaalika Arsenal uwanjani ambao wameshinda mechi 11 na kupoteza moja pekee kati ya mechi 15 za nyumbani msimu huu.
Fulham, licha ya hima na kujikaza moyo konde baada ya kucharazwa 5-0 na Manchester City juma lililopita, walibaki wakikondolea janga la kushuka daraja baada ya kusalia wavuta mkia huku kukiwa zikisalia mechi sita.
0 comments:
Post a Comment