YANGA SC imekamilisha ziara yake ya Kanda ya Ziwa kwa sare ya bila kufungana na wenyeji Rhino FC iliyopanda Ligi Kuu msimu huu kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora jioni hii.
Pamoja na sare hiyo, Yanga SC ilishindwa kucheza vyema kwenye Uwanja huo dhidi ya wenyeji, Rhino timu inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kutokana na ubovu wa Uwanja.
Mabingwa hao wa Bara, pamoja na hali hiyo mbovu ya Uwanja walijitahidi kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga mabao, lakini washambuliaji wake waliendeleza kile kinachojulikana mbele ya wapenzi wao, kushindwa kutumbukzia mipira nyavuni.
Wote Didier Kavumbangu, Jerry Tegete, Shaaban Kondo na Said Bahanuzi walikosa mabao ambayo huwezi kuamini, na kutokana na ukweli kwamba hao ndio washambuliaji pekee wa timu hiyo, maana yake wanahitaji kuboresha safu hiyo.
Awali, katika ziara hiyo ya kujiandaa na msimu mpya, Yanga inayofundishwa na kocha Mholanzi, Ernie Brandts ilitoka sare ya 1-1 mjini Mwanza Julai 6 na Express ya Uganda kabla ya kufungwa 2-1 mjini Shinyanga na timu hiyo siku iliyofuata.
Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, bao la Yanga lilifungwa na kiungo Hamisi Thabit aliyesajiliwa kutoka African Lyon dakika ya 40, wakati Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, bao la kufutia machozi lilifungwa na Shaaban Kondo, baada ya mpira wa kurushwa wa Mbuyu Twite.
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Rajab Zahir/Ibrahim Job, Mbuyu Twite, Salum Telela, Nizar Khalfan, Hamisi Thabit/Abdallah Mnguli, Didier Kavumbangu, Jerry Tegete/Shaaban Kondo na Said Bahanuzi.
0 comments:
Post a Comment