Home
»
Unlabelled
» CHADEMA WANATAKA KUINUA MICHEZO TANZANIA
Kutokana
na tukio la kinyama lililotokea Arusha, sitaweza kusoma hotuba ya
Bajeti Kivuli Bungeni. Wabunge wote wa CHADEMA tunaenda Arusha
kuomboleza, kutafakari na kuwapa moyo watanzania wenzetu. Kufuatia
matokeo ya mchezo wa leo dhidi ya Ivory Coast, nimeona niwamegee kile
ningesema kuhusu Michezo. Soma natafakari.
MAENDELEO YA MICHEZO
Mheshimiwa Spika, maendeleo mazuri ya michezo katika taifa lolote, ni
utambulisho mzuri wa taifa hilo katika mataifa mengine kutokana na
ushirikiano wa kimichezo na mataifa hayo. Pamoja na mambo mengine,
michezo katika nchi yetu inaweza kutumika kutengeneza fursa za kiuchumi
kwa kuitangaza nchi yetu duniani katika sekta za utalii na uwekezaji.
Ukiacha mbali suala la manufaa ya kiuchumi yanayoweza kupatikana kupitia
michezo, michezo pia inawajengea vijana wetu afya na hivyo kuwa na
taifa la watu wakakamavu. Kwa upande mwingine, michezo pia ni ajira.
Inasikitisha kwamba katika hotuba nzima ya Waziri wa Fedha, hapakuwa na
mpango wowote wa kukuza michezo hapa nchini bila hata kujali kwamba timu
yetu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ipo katika nafasi nzuri sana hivi sasa
kuliko wakati mwingine wowote katika kuweza kufuzu kucheza fainali za
kombe la Dunia mwakani.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Bunge ya
Maendeleo ya Jamii katika barua yake ya tarehe 5/4/2013 iliomba Kamati
ya Bajeti kuangalia namna ya kusaidia kupata fedha za kujenga michezo na
hasa kusaidia Taifa Stars katika juhudi zake za kuelekea kufuzu kwenye
michuano ya kombe la Dunia huko Brazil.
Hata hivyo Wizara ya Fedha
haikutoa hata senti tano kwa ajili hiyo. Kamwe hatuwezi kufanikiwa
kwenye michezo bila kuwekeza na kutegemea juhudi za dharura za kamati za
kusaidia ushindi. Tukitaka tung’ae kwenye michezo ni lazima tuwekeze
sana na kuwekeza ni gharama, gharama ambayo thamani yake ni kubwa sana
kwa nchi.
Mheshimiwa Spika, licha ya michezo kuliingizia taifa
mapato kupitia asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
inayotokana na viingilio katika michezo mbalimbali, hakuna uwekezaji
wowote wa maana uliofanyika kwenye michezo jambo ambalo ni hatari kwa
uhai na maendeleo ya michezo hapa nchini. Aidha hakuna mipango madhubuti
ya muda mrefu kuhusu maendeleo ya michezo hapa nchini.
Kutowepo
kwa mipango madhubuti na ya muda mrefu, kumeshababisha timu zetu kufanya
vibaya katika mashindano mengi ya kimataifa na hivyo kulifanya taifa
letu lionekane kuwa ni taifa dhaifu au kichwa cha mwendawazimu kama
alivyopata kusema Rais Mstaafu was Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan
Mwinyi.
Kambi Rasmi ya Upinzani, inatoa angalizo kwa Serikali kwamba,
kamwe hatuwezi kufanikiwa katika michezo kwa mipango ya kukurupuka.
Aidha ni aibu kwa Serikali kukusanya kodi kutokana na michezo, halafu
vijana wetu wanakosa fedha ya nauli kwenda nchi nyingine kwa mashindano
ya michezo mpaka wafanye harambee ya kukusanya fedha kwa wahisani.
Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA
inapendekeza mambo yafuatayo yafanyike ili kunusuru tasnia ya michezo
hapa nchini;
1. Timu yoyote itakayowakilisha taifa katika mashindano yoyote ya kimichezo igharamiwe na Serikali kwa asilimia 100.
2. Viwanja vyote vya Michezo hapa nchini viundiwe Wakala wa Serikali,
Wakala wa maendeleo ya michezo (Sports Development Agency). Wakala huo
uwe na majukumu ya kujenga viwanja vipya na kusimamia viwanja hivyo kwa
niaba ya Serikali. Viwanja vyote vya michezo vilivyoporwa na CCM kama
Lake Tanganyika – Kigoma, Ali Hasan Mwinyi - Tabora, Kirumba – Mwanza,
Maji Maji – Songea nk virejeshwe Serikalini mara moja chini ya Wakala wa
Viwanja vya Michezo. Wakala pia ujenge academies za michezo maeneo kama
vile Mbeya, Tanga, Mtwara, Mwanza, Manyara na Dar es Salaam ili kukuza
vipaji vya watoto na vijana.
3. Mashirika yote ya Umma, hasa
mashirika makubwa yawe na timu za michezo. Ushauri uliotolewa na IMF na
Benki ya Dunia dhidi ya Mashirika ya Umma kuwa na timu ulikuwa ushauri
usio wa maana. Wenzetu Uganda kwa mfano, Mamlaka ya Mapato Uganda (URA)
wana timu katika ligi Kuu, ambayo ni moja ya timu mahiri katika ukanda
huu wa bara la Afrika.
4. Serikali ianzishe Mfuko Maalum wa Michezo
(Sports Fund). Pia, Serikali ianzishe Kodi ya Maendeleo ya Michezo
(Sports Development Levy). Kodi hii ipatikane kama ifuatavyo: Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) ya asilimia 18 iliyokuwa ikikatwa kwenye
viingilio katika michezo mbalimbali iondolewe na badala yake kiasi
hichohicho kiingizwe kwenye Mfuko wa Michezo (Sports Fund)
utakaoanzishwa.
5. Matumizi ya Mfuko wa michezo yawe kama ifuatavyo:
i. Asilimia 50 ya fedha zitakazokusanywa zitumike kujenga miundombinu
ya michezo (Sports Infrastructure) kupitia kwa Wakala wa Maendeleo ya
Michezo na Academies. ii. Asilimia 50 inayosalia itumike kuhudumia maandalizi ya timu za Taifa.
0 comments:
Post a Comment