Searching...
Image and video hosting by TinyPic
23 February 2015
Monday, February 23, 2015

Mkutano wa matawi ya Simba waandaliwa.


Na Oscar Oscar Jr

Baada ya timu ya Simba kupoteza mchezo wa ligi kuu mbele ya Stand United ya Shinyanga kwa bao 1-0 hapo jana, mashabiki na baadhi ya wanachama wameonekana kutofurahia mwenendo wa timu yao na tayari kuna taarifa za kuitisha mkutano wa matawi yote ya timu hiyo ili kujadili kwa kina sababu zinazopelekea kusua sua kwa timu hiyo.

Baada ya timu hiyo kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Mapinduzi huko visiwani Zanzibar na kushinda mchezo wake uliofuata dhidi ya Ndanda Fc, matumaini ya timu hiyo yalikuwa makubwa sana huku watu wengi wakiamini kikosi hicho chini ya kocha Goran Kopunovic, kingeweza kurejesha heshima ambayo wanamsimbazi wameikosa kwa muda lakini kwa mwenendo huu, wengi wameanza kukata tamaa.

Simba ambayo imeshuka dimbani msimu huu mara 15, imepata ushindi mara nne, ktoka sare mara nane na kupoteza mara tatu. Haya sio matokeo mazuri kutokana na uwekezaji uliofanywa kwenye kikosi hicho. 

Simba pia inaripotiwa kuwa na mgogoro wa ndani kwa ndani kwenye Uongozi hali inayopelekea kuathiri pia uwezo wa wachezaji uwanjani.

Mwenyekiti wa tawi la Simba la Home Boyz, Hassan Kaniki amezungumza na E-SPORTS ya EFM na kueleza kuwa wao hawafurahii mwenendo mzima wa timu yao na sasa wanataka kuitisha mkutano wa matawi yote ya Simba ili kuweza kung'amua matatizo ya timu yao na kujaribu kutafuta suluhisho.

Kabla ya timu kupoteza mchezo wao dhidi ya Stand United, kuna habari zilitoka ingawa hazikuthibitishwa kuwa walipotoka sare na Coastal Union kulikuwa na mgororo wa Uongozi ambao ulipelekea timu kushindwa kulipa gharama za Hotel waliyofikia Jijini Tanga kwa muda muafaka lakini baadaye mambo yakatengemaa baada ya kupata ushindi dhidi ya timu ya Polis Moro.

Bado simba wana nafasi ya kujipanga upya na kufanya vizuri ingawa uwezekano wa timu hiyo kuweza kumaliza kwenye moja ya nafasi mbili za juu ili kuweza kupata nafasi ya kucheza mechi za kimataifa barani Afrika ni mdogo mno.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!