Searching...
Image and video hosting by TinyPic
6 August 2014
Wednesday, August 06, 2014

Asante na kwaheri Xavi Hernandez



Na Chicoti jr (Cico cicod) 
 0755 7000 76

Miaka kama mitatu iliyopita mwanaume mmoja toka mji wa Govan pale kwa Waskotish mikono ilimtetemeka, macho yalimtoka hakuamini alichokuwa anakiona baada ya kukutana na ubora wa vijana toka la masia pale Barcelona nazungumzia Jumamosi ya Mei 28, 2011 pale Wembley, Fainali ya mabingwa wa ulaya kati ya Barcelona dhidi ya Manchester United, Sir Alex Ferguson dhidi ya Pep Guardiola. 

Ni katika usiku huo ndipo Kibabu Fergie alitamka bila kutafuna maneno “katika maisha yangu ya kufundisha soka sijawahi kukutana na timu bora kama hii” ulitaka aseme nini zaidi kwa ubora wa Messi, Xavi na Iniesta wakichagiza mtindo wa “tiki taka”. Kama ni kilele cha Mlima Kilimanjaro basi Barcelona ya Pep na la masia ilifika kibo na mawenzi usiku ule pale Wembley. 

Siri ya mafanikio ya mfumo wa “tiki taka” pale Barcelona na Hispania nyuma yake alikuwa mwanaume aliyeitwa XAVI HERNANDEZ, hakuwa na miguu ya Messi, chenga za Iniesta wala nguvu za Yaya Toure lakini yeye ndiye aliyeamua mpira uende wapi, kwa wakati gani na kwa nani, silaha yake kubwa ikiwa ni kupiga pasi za uhakika. 

Baada ya kucheza mechi 133 za timu ya Hispania maarufu kama “la roja” hatimaye Xavi Hernandez ameamua kustaafu kuichezea timu ya taifa, alikuwa sehemu ya kizazi cha Hispania kilichonyakuwa kombe la ulaya pale Vienna mwaka 2008 baada ya miaka 44 bila kombe na baadaye 2010 kunyakua kombe la dunia nchini Afrika ya kusini na kunyakuwa tena kombe la ulaya 2012 hii inamaana anastaafu bila deni dhidi ya Wahispania. 

Kuonyesha ni kwa jinsi gani alikubalika mwaka 2010 kwenye mechi ya nusu fainali ya kombe la Dunia pale Afrika ya Kusini dhidi ya Ujerumani dakika 2 kabla ya mpira kuisha refa alimwambia “naweza kuipata jezi yako baada ya mechi” na Xavi alimjibu “kama utaweza kupuliza filimbi ya kumaliza mchezo mapema zaidi, jezi ni yako”. 

Katika umri wa miaka 34 miguu ya Xavi haina kasi tena na sasa ameamua kujikita pale Barcelona kabla hajaachana kabisa na soka, ila atabaki kukumbukwa kama mpiga pasi hodari na mahiri katika dunia ya soka lijulikanalo kama “sexy football”. Niseme tena Asante na kwaheri Xavi.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!