Searching...
Image and video hosting by TinyPic
2 January 2015
Friday, January 02, 2015

Uchambuzi: Ruvu Shooting vs Kagera Sugar


Na Oscar Oscar Jr

Baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wanajeshi wenzao, timu ya Ruvu Shooting chini ya kocha Tom Olaba leo inajiandaa kushuka dimbani kumenyana na vijana wa Kagera Sugar ambao nao wametoka kupata ushindi kama huo mbele ya timu ya Simba kwenye mechi za mzunguko wa nane ligi kuu Tanzania bara.

Siri kubwa ya mafanikio ya Kagera Sugar msimu huu, ni namna kocha wa timu hiyo alivyoifanya kuwa na safu bora ya Ulinzi ambapo mpaka sasa, ni wao na vinara wa ligi hiyo timu ya Mtibwa Sugar ndiyo wameruhusu mabao machache kwenye ligi (Kila moja imefungwa mabao manne tu).

Kagera Sugar inaonekana pia kuwa na Safu ya ushambuliaji yenye uwezo kwani mpaka sasa imefunga mabao saba huku mabao manne yakifungwa na mchezaji mmoja, Rashidi Mandawa.

Ruvu Shooting ambao wanaelekea kwenye mchezo huo huku wakiwa wamepoteza michezo minne msimu huu, watakuwa na kila sababu ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo hasa ukizingatia kuwa wanacheza nyumbani kule Mabatini-Pwani.

Kuelekea mchezo huo, Kagera wanaonekana kuwa na rekodi nzuri msimu huu hususani mbele ya timu kongwe kwenye ligi kwani tayari wamefanikiwa kuzifunga timu za Yanga na Simba na kutoka sare na vinara wa ligi hiyo, Mtibwa Sugar. 

Pengine rekodi na ubora wa kikosi hicho, inaweza kuwa mwiba mchungu kwa Ruvu Shooting ambao bado hawajaonekana kama ni tishio msimu huu kwani wameshinda michezo mitatu pekee.

Kueleka mchezo huu, Ruvu Shooting wanakwenda wakiwa kwenye nafasi ya nane baada ya kujikusanyia alama 10 kwenye msimamo wa ligi kuu, huku Kagera Sugar wao wakishika nafasi ya nne baada ya kutimiza pointi 13.

Endapo Kagera Sugar wataibuka na ushindi kwenye mchezo huo wa kuanzia mabao manne, wataongoza ligi kwa muda kwani watafikisha pointi 16 ambazo zimefikishwa na Mtibwa Sugar ambao wako kwenye mashindano ya Mapinduzi huko visiwani Zanzibar.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!