Searching...
Image and video hosting by TinyPic
2 January 2015
Friday, January 02, 2015

Uchambuzi: Coastal Union vs Ruvu JKT


 Na Oscar Oscar Jr

Katika Dimba la Mkwakwani pale Jijini Tanga, Jumamosi ya leo utafanyika mchezo mmoja wa ligi kuu Tanzania bara ambapo wenyeji Coastal Union watawaalika maafande wa JKT Ruvu kutoka mkoa wa Pwani. 

Coastal Union baada ya kulazimishwa sare pacha na Tanzania Prisons kule Sokoine juma lililopita, watawavaa wanajeshi hao ambao wanaugulia maumivu ya kutandikwa bao 1-0 na ndugu zao Ruvu Shooting kwenye mchezo uliopita.

Pamoja na kupoteza mchezo uliopita, bado JKT Ruvu ni timu inayoonyesha upambanaji uwanjani na kutengeneza nafasi nyingi sana za kufunga na pengine kitu kinachowanyima kupata magoli mengi, ni kukosa umakini tu ingawa wana magoli saba mpaka sasa

Ukitazama ubora wa safu za ulinzi wa timu hizi, bado hakuna tofauti kubwa kwani Coastal Union wamesharuhusu mabao saba kufungwa huku Ruvu JKT wao wakiruhusu mabao nane.

Kazi kubwa ambayo walinzi wa Ruvu JKT watakayokuwa nayo ni kuhakikisha wanamzuia mshambuliaji hatari wa Coastal Union, Ramadhan Salim endapo ataanza kwenye mchezo huo kwani mpaka sasa ameshapachika mabao manne wavuni.

Kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo Yussuph Chippo, na nafasi yake kuchukuliwa na James Nandwa bado hakujaonyesha mapungufu yoyote licha ya mchezo wa kwanza wa James kama kocha mkuu timu hiyo ilitoka sare.

Katika mchezo huo, Coastal Union hawakuonyesha kiwango kizuri sana kiuchezaji pengine ni kutokana na ubovu wa Uwanja wa Sokoine ambao ulikuwa umejaa matope kutokana na mvua kunyesha siku hiyo kwa kiwango kikubwa.

Coastal Union wanaelekea kwenye mchezo wa leo huku wakiwa na alama 12 wakishika nafasi ya tano na endapo wataibuka na ushindi, watapanda hadi nafasi ya pili kwani watatimiza alama 15 na kuzishusha timu za Yanga na Azama ambazo zinapointi 14 kila mmoja huku timu hizo zikiwa visiwani Zanzibar kwenye michuano ya Mapinduzi.

Kwa upande wa Ruvu JKT, wao wanakwenda kwenye mchezo huu wakiwa kwenye nafasi ya saba wakiwa na alama 10 na kama wataibuka na ushindi wanaweza kusogea hadi kwenye nafasi ya tano huku wakisubiria matokeo ya Kagera Sugar ambao wana alama 13 nao watakuwaa dimbani ili kuamua yupi ashike nafasi ya nne na mwingine ya tano.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!