Searching...
Image and video hosting by TinyPic
16 January 2015
Friday, January 16, 2015

Uchambuzi: QPR vs Manchester United.


Na Chikoti Cico

Kwenye uwanja wa Loftus Road siku ya Jumamosi saa 12 jioni wenyeji timu ya QPR wataikaribisha Manchester United katika moja ya mechi za ligi kuu nchini Uingereza mchezo unaotarajiwa kuwa wa vuta nikuvute huku kila timu ikitaka kunyakua alama tatu muhimu.

QPR inayoshika nafasi ya 19 kwenye msimamo wa ligi huku ikiwa na alama 19 inahitaji kucheza kufa na kupona kushinda mchezo huo na kupata alama tatu muhimu ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kuondoka katika hatari ya kushuka daraja kwenye msimamo wa ligi.

Kocha wa QPR Harry Redknapp ambaye yuko kwenye hatihati ya kufukuzwa kazi kutokana na mwenendo mbaya wa klabu hiyo, kwenye mchezo huo atawakosa Armand Traore, Sandro na Yun Suk-Young ambao ni majeruhi.

Kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha katika michezo 16 iliyopita katika mashindano mbalimbali dhidi ya Man United, QPR wamefungwa michezo 13 na kutoka sare michezo mitatu.

Pia takwimu zinaonyesha katika michezo tisa iliyopita QPR waliyocheza na United katika mashindano mbalimbali kwenye uwanja wa Loftus road wamefungwa michezo sita na kutoka sare michezo mitatu.

Kikosi cha QPR kinaweza kuwa hivi: Green; Isla, Caulker, Dunne, Hill; Vargas, Barton, Henry, Fer; Zamora, Austin

Kwa upande wa Manchester United mshambuliaji Robin van Persie ana nafasi ndogo ya kucheza mchezo huo baada ya kupata majeraha ya kifundo cha mguu kwenye mchezo dhidi ya Southampton hivyo Radamel Falcao ama James Wilson mmojawapo ataiongoza safu ya ushambuliaji ya United kwenye mchezo huo.

Naye Ashley Young ambaye ni majeruhi atakosekana kwenye mchezo huo huku mabeki Marcos Rojo na Rafael ambao wamepona majeraha yao wakiwa na nafasi ya kucheza mchezo huo.

Kocha wa Manchester United Louis van Gaal ambaye ana kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo uliopita kwa kufungwa na Southampton kwa goli 1-0 nyumbani Old Trafford matokeo yaliyopelekea timu yake kushuka mpaka nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 37.

Hivyo kwenye mchezo dhidi ya QPR, Van Gaal atataka kupata alama tatu muhimu ili kuendelea kujihakikishia nafasi kati ya timu nne za juu (top four).

Kwa upande wa Manchester United takwimu zinaonyesha katika michezo 19 iliyopita ya ligi ambayo United imecheza katika jiji la London imeshinda michezo 11 na kufungwa mchezo mmoja huku ikitoka sare michezo saba.

Pia takwimu zinaonyesha mshambuliaji wa United Wayne Roney amehusika katika magoli matano katika michezo minne aliyoanza dhidi ya QPR kwenye ligi huku akifunga magoli matatu na kutoa pasi mbili za magoli (assist).

Kikosi cha Manchester United kinaweza kuwa hivi: De Gea; Jones, Smalling, Blind; Valencia, Carrick, Fellaini, Di Maria, Shaw; Rooney, Falcao

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!