Searching...
Image and video hosting by TinyPic
16 January 2015
Friday, January 16, 2015

MAKALA: Afrika yetu, AFCON yetu, Soka letu.


Na Chikoti Cico
 
Ndivyo unavyoweza kusema kuelekea michuano mikubwa ya soka barani Afrika yaani kombe la Mataifa ya Afrika, “Afrika yetu, AFCON yetu, soka letu” kila tunachoenda kushuhudia Guinea ya Ikweta ni cha kwetu.

Ikiwa ni michuano ya 30 toka kuanzishwa kwa michuano hii mikubwa barani Afrika, mataifa 16 yataumana katika viwanja mbalimbali katika miji ya Bata, Malabo, mongomo na Ebebiyin nchini Guinea ya Ikweta katika kutafuta mfalme mmoja wa bara hili lenye watu zaidi ya bilioni moja.

Mataifa 16 yatakayoshiriki kwenye kinyang’anyiro hicho ni wenyewe Guinea ya Ikweta, Afrika ya Kusini, Kongo, Algeria, Mali, Gabon, Burkina Faso, Kameruni, Ivory Coast, Ghana, Guinea, Cape Verde, Zambia, Tunisia, Senegal na DR Kongo

Kuelekea kwenye michuano hiyo itakayoanza tarehe 17 Januari siku ya Jumamosi ni muhimu kwa Waafrika kuja pamoja kushiriki michuano hii iwe ni kwa kuhudhuria uwanjani hasa kwa wale ambao wanaweza kufanya hivyo ama kwa kutazama kupitia vyombo vya mbalimbali vya habari au kwa kupeana taarifa kupitia mitandao ya kijamii vyovyote vile ni lazima tujivunie michuano hii.

Pamoja na kwamba Waafrika wengi tumekuwa wafwatiliaji wazuri wa ligi za Ulaya na michuano ya mabara mengine lakini huu ni muda wetu sasa kujivunia kilicho chetu, kujivunia wachezaji wetu, kujivunia soka letu, kujivunia utamaduni wetu, na kujivunia bara letu kwasababu michuano hii ni utambulisho wa bara letu la Afrika.

Michuano hii itahusisha wachezaji wengi mashuhuri kutoka barani Afrika ambao wanatamba katika ligi mbalimbali duniani kama vile mchezaji bora wa Afrika kwa mwaka 2014 Yaya Toure (Ivory Coast), Wilfried Bony (Ivory Coast), Asamoah Gyan (Ghana), Andre Ayew (Ghana), Papiss Cisse (Senegal), Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon), Jonathan Pitroipa (Burkina Faso), Yacine Brahimi (Algeria) 

Katika kuwashangilia wachezaji hao na timu zao huu ndiyo wakati wa kuimba nyimbo zetu za taifa kwa ushujaa na kwa kujivunia kuwa sehemu ya bara hili, huu ndiyo wakati wa kujichora miili yetu kwa bendera za nchi yetu na huu ndiyo wakati wa kupiga ngoma zetu kuonyesha furaha na umahiri wetu katika kuzishangilia timu shiriki kwa wiki tatu za michuano hiyo ya AFCON.

Pamoja na kwamba ugonjwa hatari wa Ebola ulihatarisha michuano hii kufanyika na kupelekea wenyeji wa kwanza wa michuano hii nchi ya Morocco kujitoa katika kuandaa kabla ya Guinea Ikweta kuchukua jukumu la kuandaa michuano hii lakini bado ni muhimu kwa kila anayehusika kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo kwa wakati wote wa michuano hiyo.

Mwisho nimalizie kwa kauli hii maarufu miongoni mwa watu wengi duniani kote “They call it Africa, we call it home” ikimaanisha “wanapaita Afrika, tunapaita nyumbani”
NAWASILISHA.


0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!