Searching...
Image and video hosting by TinyPic
19 January 2015
Monday, January 19, 2015

Leo ni Liverpool vs Chelsea saa 4:45 usiku.


Na Chikoti Cico


Usiku wa leo kwenye uwanja wa Anfield kutakuwa na mtanange wa kukata na shoka kati ya Liverpool dhidi ya Chelsea katika nusu fainali ya kwanza ya kombe la Capital One, mchezo unaotarajiwa kuwa wa kusisimua hasa ikizingatiwa kwamba kila timu inataka kuchukua kombe hilo na kuwapa raha mashabiki wake.

Timu ya Liverpool ambayo mpaka sasa imecheza michezo minane katika mashindano mbalimbali bila kupoteza mchezo wowote inatarajiwa kucheza kwa nguvu kwenye mchezo huo kutafuta ushindi ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kuingia fainali.

Timu ya Liverpool ambayo mpaka sasa haijanyakua kombe lolote chini ya kocha Brendan Rodgers kwenye mchezo huo inatarajiwa kumrejesha kikosi nahodha wa klabu hiyo Steven Gerrard ambaye hakucheza mchezo uliopita dhidi ya Aston Villa baada ya kupata majeraha ya kukaza kwa ukano wa mvungu wa goti (hamstring).

Huku wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kufungwa kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya ligi kwa magoli 2-1 klabu ya Liverpool itahitaji kuwa kwenye kiwango bora kabisa kwenye mchezo huo ili kuweza kujipatia ushindi.

Brendan Rodgers ambaye alikuwa sehemu ya benchi la ufundi la klabu ya Chelsea kuanzia mwaka 2004-2006 kuelekea mchezo huo wa Capital One takwimu zinaonyesha kocha huyo amepoteza michezo yote mitatu aliyocheza dhidi ya Chelsea akiwa kocha wa Liverpool.

Nayo klabu ya Chelsea ambayo inaongoza kwenye msimamo wa ligi ya Uingereza huku ikishinda kwa jumla ya magoli 5-0 dhidi ya Swansea Jumamosi iliyopita inatarajiwa kucheza kufa na kupona ili kupata matokeo mazuri na kujitengenezea njia ya kufika fainali.

Kocha wa Chelsea Jose Mourinho kwenye mchezo huo anaweza kufanya mabadiliko machache huku Thibaus Courtois, Kurt Zouma, Loic Remy na Andre Schurrle wakitarajiwa kupata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza.

Kuelekea mchezo huo Mourinho anaonekana kuwa na rekodi nzuri dhidi ya Liverpool huku katika michezo 19 akishinda michezo 10 na kufungwa michezo mitano huku akitoka sare michezo minne.

Nani ataibuka mbabe kwenye mchezo huo? na nani atakwenda Wembley kucheza fainali ya Capital One? Majibu ya maswali yote hayo yatajulikana baada ya michezo miwili ya nusu fainali ya kombe hilo huku mmoja ukiwa ni leo usiku kati ya “The reds vs The blues” pale Anfield.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!