Na Oscar Oscar Jr
Baada ya kutoka sare kwenye mchezo wao wa tisa kwenye ligi kuu Tanzania bara, Stand United ambao wako mkoani Pwani maeneo ya Mlandizi kwa kambi ya muda mfupi, wanajiandaa kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wao wa mzunguko wa 10 ambapo watashuka dimbani kupambana na JKT Ruvu.
Timu ya JKT Ruvu ambayo imetoka kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union kwenye dimba la Mkwakwani, watawaalika vijana hao maarufu kwa jina la Chama la Wana tarehe 10 majira ya saa 10:30.
Stand ambao hawajapoteza mchezo hata mmoja ugenini, watamkosa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Harouna Chanongo ambaye alipewa kadi nyekundu kwenye mzecho wao dhidi ya Polis Morogoro ambapo mchezo ulimalizika kwa timu hizo kutoka sare pacha.
Akizungumza na mtandao huu msemaji wa timu hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Bilal alisema" Pamoja na Chanongo kuukosa mchezo wetu dhidi ya JKT Ruvu, bado hatuna wasiwasi kwani hata kabla hatujamsajili, kuna mtu alikuwa anacheza kwenye nafasi hiyo"
Alipoulizwa kama kadi ile ilikuwa halali au mwamuzi aliitoa kimakosa, Bilal anasema "Hatuwezi kulalamika sana kuhusiana na kadi ile ingawa hakukuwa na madhambi makubwa ya kumfanya mwamuzi ampe kadi lakini tumeichukulia kama changamoto kwetu"
Harouna Chanongo amabaye alisajiliwa kwa mkopo na Stand United akitokea klabu ya Simba amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Stand na kumkosa mchezaji huyo kwenye mchezo wao dhidi ya JKT Ruvu ni pigo japo Stand wamegoma kukiri hilo.
0 comments:
Post a Comment