Hatimaye Mnyama ameunguruma Zanzibar
Na Florence George.
Pamoja na kutoa vituko vya hapa na pale, kocha mpya wa Simba Goran Kopunovic ameweza kuiongoza timu hiyo kutinga kwenye hatua ya robo fainali ya Mapinduzi Cup huko Zanzibar baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo uliowakutanisha na timu ya JKU.
Bao pekee lililofungwa na Ramadhani Singano lilitosha kuamsha matarumbeta ya watoto hao wa mtaa wa Msimbazi katikati ya Jiji la Dar es salam ambapo sasa wametimiza pointi sita na kuongoza kundi lao huku wakifuatiwa na Mtibwa Sugar wenye alama tano, JKU pointi nne na mafunzo wakiondolewa baada ya kupata alama moje pekee.
Katika mchezo wao wa leo walionekana kutulia na kutandaza soka safi kupitia viungo Jonas Mkude, Said Ndemla na Ramadhani Singano amabaye alikuwa anafanya kazi nzuri sana katika kuanzisha mashambulizi huku mara kadhaa akipitia katikati badala ya pembeni ambapo wengi wamemzoea.
Mabeki Mohamed Hussein na Ramadhani Kessy kwa upande wa Simba, walionekana imara sana huku wakishambulia kwa muda mrefu kutokana na kucheza bila tahadhari yoyote hasa ukizingatia kuwa JKU walionekana kuchezea mpira kwa pasi fupi fupi ambazo hazikuwa na madhara kwenye lango la Simba.
Huenda huu ukawa ni mwanzo mzuri kwa Simba ambao wanaonekana kutofanya vizuri kwenye ligi kuu na baada ya kufungwa na Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa kwanza wa michuano hii, hofu ilitawala lakini chini ya kocha Kopunovic mambo yanaonekana kuwa shwari.
0 comments:
Post a Comment