Searching...
Image and video hosting by TinyPic
2 December 2014
Tuesday, December 02, 2014

Uchambuzi: Sunderland vs Manchester City


Na Chikoti Cico.

Kivumbi cha ligi kuu nchini Uingereza kitatimka siku ya Jumatano kwenye uwanja wa Stadium of Light, pale timu ya Sunderland itakapoikaribisha timu ya Manchester City mchezo unaotarajiwa kuwa wa kukata na shoka huku kila timu ikitafuta alama tatu muhimu.

Timu ya Sunderland inayofundishwa na kocha Gus Poyet, inatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo kutafuta ushindi wa tatu muhimu kwenye ligi hiyo kwani mpaka sasa wameshinda michezo miwili peke yake huku wakitoka sare michezo nane.

Mpaka sasa Sunderland inashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 14 baada ya kucheza michezo 13 toka kuanza kwa msimu wa ligi kuu nchini Uingereza, kuelekea kwenye mchezo dhidi ya City Sunderland watawakosa Emanuele Giaccherini, Billy Jones, na Patrick van Aanholt ambao ni majeruhi.

Takwimu zinaonyesha Sunderland wamekuwa na rekodi nzuri dhidi ya Manchester City kwa siku za karibuni kwani katika michezo sita waliyocheza na City wameshinda michezo mitatu, kutoka sare michezo miwili na kufungwa mchezo mmoja tu.

Kikosi cha Sunderland kinaweza kuwa hivi: Pantilimon; Vergini, O'Shea, Brown, Reveillere; Cattermole, Rodwell; Johnson, Larsson, Wickham; Fletcher

Kuelekea mchezo huo dhidi ya Sunderland timu ya Manchester City baada ya kushinda mchezo uliopita dhidi ya Southampton kwa magoli 3-0 wameweza kufikisha alama 27 na kushika nafasi ya pili hivyo kuikaribia Chelsea ambao ndiyo vinara.

Manchester City inayofundishwa na kocha Manuel Pellegrini, itamkosa beki wake mahiri Vicent Kompany aliyeumia kwenye mchezo dhidi ya Southampton pia itamkosa Eliaquim Mangala aliyeonyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo huo.

Hivyo beki ya katikati ya City itaweza kuundwa na Sagna ama Boyata ili kushirikiana na Demichelis, ukiachana na Kompany na Mangala City pia wataendelea kuwakosa David Silva, Edin Dzeko na Aleksandar Kolarov ambao bado ni majeruhi.

Takwimu zinaonyesha Manchester City wamekuwa wakipata wakati mgumu kila wanapocheza na Sunderland kwenye uwanja wao wa Stadium of Light kwani katika michezo mitano wameshindwa kupata kushinda hata mechi moja.

Rekodi zinaonyesha kuwa Manchester City wamefungwa michezo minne ya mwisho mfululizo na kutoka sare mara moja. pia takwimu zinaonyesha kiungo wa City, James Milner ameifunga Sunderland magoli mengi kuliko timu nyingine yoyote, Milner ameifunga Sunderland magoli matano.

Kikosi cha Manchester City kinaweza kuwa hivi: Hart, Zabaleta, Demichelis, Boyata, Clichy, Toure, Fernandinho, Lampard, Nasri, Navas, Aguero

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!