Searching...
Image and video hosting by TinyPic
10 December 2014
Wednesday, December 10, 2014

Uchambuzi: Roma vs Manchester City


Na Chikoti Cico.

Moja ya mechi za kumalizia mzunguko wa mwisho wa ligi ya mabingwa Ulaya yenye msisimko ni ile itakayopigwa kwenye uwanja wa Stadio Olimpico kati ya AS Roma dhidi ya Manchester City.

Timu zote mbili zinaingia kwenye mchezo huo zikiwa na nafasi ya kuvuka hatua ya makundi huku kila mmoja akihitaji kushinda mchezo huo.

AS Roma wanatarajia kuingia kwenye mchezo huo kutafuta ushindi kwa nguvu zote ili kujihakikishia nafasi ya kuvuka hatua ya makundi kwani mpaka sasa wanashika nafasi ya pili wakiwa na alama tano sawa na City na CSKA Moscow wanaocheza na Bayern Munich katika mchezo mwingine wa kundi E.

Kocha wa AS Roma Rudi Garcia baada ya kuwapumzisha Gervinho, Ashley Cole na nahodha Francesco Totti kwenye wa ligi ya Italia dhidi ya Sassuolo mwishoni mwa wiki ulioisha kwa sare ya magoli 2-2 ataweza kuwatumia wachezaji hao kutafuta alama tatu muhimu dhidi ya City.

Takwimu zinaonyesha timu ya Roma imeshinda katika michezo mitatu iliyopita dhidi ya timu kutoka Uingereza waliyocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Kikosi cha AS Roma kinaweza kuwa hivi: De Sanctis; Florenzi, Manolas, Astori, Cholevas, Nainggolan, De Rossi, Keita, Gervinho, Totti, Ljajic.

Timu ya Manchester City wao wana presha kubwa zaidi kuelekea mchezo huo kwani mpaka sasa wanashika nafasi ya tatu wakiwa na alama tano huku wakiombea CSKA Moscow wafungwe na Bayern Munich halafu wao washinde ama kutoka sare ya bila kufungana na Roma ili waweze kuvuka hatua ya makundi.

Kocha wa Manchester City Manuel Pellegrini ataingia kwenye mchezo huo bila ya mshambuliaji wake Sergio Aguero aliyeumia kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Everton.

Pia atamkosa kiungo Yaya Toure ambaye anatumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu huku nahodha Vicent Kompany ambaye anasumbuliwa na majeruhi akiwa na hatihati ya kutokucheza mchezo huo.

Kuelekea mchezo huo Manchester City wamekuwa na rekodi mbaya nchini Italia kwani hawajawahi kushinda mchezo wowote nchini humo huku rekodi zikionyesha kuwa wamefungwa michezo miwili na kutoka sare michezo miwili.

Kikosi cha Manchester City kinaweza kuwa hivi: Hart; Zabaleta, Demichelis, Mangala, Clichy; Fernando, Fernandinho; Navas, Nasri, Milner; Dzeko

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!