Searching...
Image and video hosting by TinyPic
9 December 2014
Tuesday, December 09, 2014

Renovado Carletto, La Saeta Rubia Ronaldo


Na Markus Mpangala 

KUNA maneno ya Kihispania; Renovado Carletto na La Saeta Rubia Ronaldo. Neno ‘Renovado’ kwa lugha ya kiingereza tungesema ‘Renew', halafu Carletto ni lile jina la utani la Carlo Ancelotti. 

Kwa lugha ya jumla ya Kiswahili tungesema Carlo Ancelotti ameongeza mkataba wake, ameongeza muda wa kuifundisha Real Madrid. 

Kwa Ronaldo kuna neno ‘La Saeta Rubia’, lakini kwa lugha ya kiingereza tungesema ‘My Way’. Kwa lugha yetu tamu kabisa ya Kiswahili tungesema ‘mwelekeo au njia’. Hii ni misingi ya mtu anapopambana kufanikiwa au kufanikisha kitu. 

Katika maisha unapambana kwa ‘staili’ yako ili uweze kushinda. Kwahiyo Ronaldo bado anapambana kwa njia yake ya kimya kimya. Kabla sijaendelea labda nisema hili; Shabiki yeyote wa Real Madrid anatakiwa kuwa mpinzani wa Lionel Messi. 

Lakini upinzani huo hauna maana kwamba utumie matusi dhidi ya mashabiki wa Messi na Barcelona. 

Tunakubali uwezo wa andunje Lionel Messi, lakini hatukubali kushindwa kupambana naye katika soka. Kwahiyo naungana na viongozi wangu wa Real Madrid kuwafungia mashabiki 17 wa klabu hiyo walioimba nyimbo za matusi na ubaguzi dhidi ya Lionel Messi. 

Sasa basi, Renovado’ aliyofanya Carlo Ancelotti kuendelea kuifundisha Real Madrid ni hatua kubwa sana. Kwanza anaongeza muda kwa Zinedine Zidane kuendelea kujifunza zaidi ukocha. Pili anataka kukamilisha ule mpango wa miaka mitano, ambao sasa umeongezwa hadi mwaka 2025 kutawala katika soka. 

Mpango huo una maana vijana kama Lucas Silva kutoka Cruzeiro, Marco Asensio kutoka Real Mallorca wataungana na vijana wengine ambao watadumu kwa mudu mrefu, Jess Rodriguez, Isco au ukimpenda muite Disco, Raphael Varane, na chipukizi wengi tu wanaokuja juu klabuni. 

Hii ina maana ‘projekti’ ya Zidane kule Castilla anazidi kusukwa huku wakati ukifika wa kupokea nafasi za akina Isco itakuwa tayari wameunganisha kikosi maridadi. Real Madrid ndiyo wajanja wa ‘town’ na Ulaya. 

Timu inapokuwa na kapteni bomba kama Sergio Ramos unategemea nini? Ramos ni mwanaume wa shoka, jabali, kiongozi, jemedari na askari wa vita yaani si mchezaji wa kuchoka. 

Jikumbushe bao lake pale Allianz Arena. Jikumbushe bao lake pale Lisboa (kwa kireno) au Lisbon pale Ureno. Kuna maneno mengi unaweza kumwelezea kuhusu Sergio Ramos mzaliwa wa pale jiji la Sevilla. 

Yupo kapteni mkuu Iker Casillas, lakini sifa kubwa ya sasa ni kuwa na Ramos ambaye wakati mwingine huamua kumfokea Casillas anapofanya makosa. Sifa zote hizo zinamfanya Carlo Ancelotti awe na viongozi wa wachezaji ndani ya dimba. 

Viongozi ambao wanaifanya timu icheze kwa kujiamini na kujituma. Pia kuwa na Cristiano Ronaldo muda wote unajisikia huru na unajua timu kabambe inaweza kuleta mabao wakati wowote. 

Kwahiyo hata njia anazotumia Ronaldo kupachika mabao ndio naweza kusema ni njia ya kipekee, ‘La Saeta Rubia. Sifa za Ronaldo si haba, tayari ametupia mabao 23 katika mechi 14 za La Liga. 

Tena timu zilizochapwa zaidi na Ronaldo ni washkaji zetu Celta de Vigo, Granada, Levante, Barcelona, Rayo, Osasuna, Valencia, Córdoba, Atletico de Madrid, Elche na Athletic Bilbao. 

Hadi naandika leo Ronaldo amefunga magoli 23 na kuzidi kuitakatisha jezi nyeupe ya Santiago Bernabeu. Hawa Celta Vigo walituadhiri awali, lakini sasa wametambua kuwa Real Madrid ni watu wa shughuli pevu. 

Kitu ambacho naweza kukufundisha leo ni kwamba, katika harakati za kupata ushindi wa Real Madrid sasa kadiri inavyowezekana pasi zinapelekwa kwa Ronaldo, faulo anaachiwa Ronaldo, na penalti anapiga Ronaldo, mabao yanapachikwa na Ronaldo. 

Mwisho wa kila mechi angalia Ronaldo amepigiwa pasi ngapi, ametoa pasi ngapi, ametengeneza mabao mangapi, amefunga mangapi na kutokea upande gani. 

Siri kubwa ni kwamba CR7 anapiga mabao kwa mashuti makali miguu yote mwili, vichwa, visigino, Looh! Natamani hata mikono ingeruhusiwa kufungia magoli eneo la penalti Hahahaaaaa! Usishangae Madridista mwenzangu. 

Hakuna kitu kizuri kama kushuhudia mambo mazuri ya timu yake. Hata ikipitia wakati mbaya utajua ni mapito ambayo yanarekebishika. Sasa watu wawili muhimu katika kikosi cha Real Madrid wameweka hewa safi. 

Yaani Ronaldo anapiga mabao na kuweka rekodi, halafu kocha ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa kiwango cha juu cha soka, Carlo Ancelotti ameongeza mkataba wa mwaka mmoja tu. 

Vyovyote itakavyokuwa, hata kama angeongeza miezi 6 tu inatosha. Wachezaji wana ‘enjoy’, mashabiki tunatabasamu kwa raha, vijana wa Castilla kule wanalo jembe Zidane. 

Tabu ya nini jamani swahiba? Real Madrid ni wafalme wa Ulaya, wapinzani wakileta uzembe, tutatetea Uefa tena msimu huu. Oooh!

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!