Searching...
Image and video hosting by TinyPic
17 December 2014
Wednesday, December 17, 2014

NIONAVYO MIMI: ASANTE PEPE KWA ZAWADI YA XMASS


 NIONAVYO MIMI: ASANTE PEPE KWA ZAWADI YA XMASS


Na Oscar Oscar Jr

Juzi wakati naanza safari ya kutoka Kampala kuelekea Nairobi, nilikuwa nasoma habari za beki wa kimataifa wa Ureno na klabu ya Real Madrid, K√©pler Laveran Lima Ferreira maarufu kwa jina la Pepe. 

Kwa kumtazama Pepe bila shaka unagundua kuwa jamaa ni bonge la muhuni, katili, hana utu na hii yote ni kutokana na matendo yake uwanjani ya vurugu ambayo mpaka sasa yamempatia kadi 12 nyekundu.

Wakati naanza safari ya kutoka Nairobi kurudi Dar es salaam, nikaanza kutafuta wachezaji bora duniani, jina la Pepe sikuliona. Nikatafuta wachezaji matajiri duniani, nako jina la Pepe sikulikuta. 

Nilipoanza kutafuta majina ya watu wanaosaidia watu wenye maisha magumu, nikakutana na jina la Pepe. Pepe ametoa msaada wa chakula kwa ajili ya sherehe za Xmass kwa watu wanaoishi maisha magumu kwenye kitongoji cha Las Rozas anakoishi nchini Hispania. 

Hataki kula Xmass peke yake, ameamua kugawana na majirani zake. Pepe hajisikii vizuri kufurahia maisha huku watu waliomzunguka wakihuzunika. Huu ni moyo wa kiuungwana kabisa.

Baada ya kukutana na uchamungu wa Pepe, nikaanza kuifuatilia habari hiyo na baaadae nikagundua kuwa, hiyo sio mara yake ya  kwanza kutoa msaada kwa watu wenye uhitaji. 

Nikapigwa na butwaa kisha nikajiuliza, hivi ni huyu Pepe anayeonekana muhuni ndiyo ana moyo wa kiuungwana kiasi hiki? sikupata jibu. Kisha nikajiuliza, hivi mimi nimewasaidia mara ngapi watu hata kipande cha sabuni? napo sikupata jibu!

Pepe sio mchezaji bora duniani, Pepe sio miongoni mwa wachezaji matajiri duniani lakini ana moyo wa kusaidia wengine. Mimi sio mchambuzi bora Tanzania, mimi sio mchambuzi tajiri Tanzania lakini moyo wangu mgumu sana kusaidia watu wengine! 

kwa mantiki hiyo, kuna uwezekano mkubwa mimi nikawa muhuni zaidi kuliko hata Pepe. Kuna uwezekano mkubwa moyo wangu pia ni mgumu kutoa kuliko wa Pepe! Wakati unauchunguza uhuni na ukatili wa Pepe, ni vema kuchunguza na uhuni wako pia!

Watu wengi tunadhani wanaopaswa kusaidia wengine ni matajiri pekee. Watu wengi tunawasema vibaya wengine huku tukikwepa wajibu wetu. Mungu nisaidie moyo wa kugawana na wenzangu hiki kidogo unachonijaalia hasa kipindi hiki cha Xmass.

Chakula alichogawa Pepe kitanufaisha familia zaidi ya 200. Pepe ametokea kwenye familia duni sana kama wengi wetu tulivyo lakini huwa hawasahau watu wake. Mwaka jana pia alifanya hivyo kwa kugawa tani tano za Chakula na mwaka huu ametoa zaidi ya tani tisa. 

Unaweza ukawa huna uwezo wa kuwapa masikini tani tisa za chakula kama Pepe lakini, kilo tano za mchele na kipande cha sabuni vinatosha kuwa Xmass kwa wenye uhitaji. Ee Mungu nijalie moyo wa kutoa. Marry xmass to you guys.

 


0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!