Searching...
Image and video hosting by TinyPic
4 November 2014
Tuesday, November 04, 2014

Uchambuzi: Maribor vs Chelsea siku ya Jumatano.


Na Chikoti Cico
 
Baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa jumla ya magoli 6-0 dhidi ya Chelsea kwenye uwanja wa Stamford Bridge timu ya Maribor itaikaribisha Chelsea kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Ljudski Vrt nchini Slovenia kwenye mchezo wa marejeano wa kundi G kwa mzunguko wa pili wa ligi ya mabingwa Ulaya.

Maribor ambao wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi G ikiwa na alama mbili katika michezo mitatu waliyocheza kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, wanatarajiwa kucheza kwa nguvu zote kwenye mchezo huo ili kupata matokeo ya kuridhisha na kufufua matumaini ya kuvuka kwenye hatua ya makundi.

Kocha wa Maribor, Ante Šimundža atamkosa beki wa katikati Aleksander Rajcevic aliyepata majeraha ya kichwa huku viungo Agim Ibraimi na Zeljko Filipovic na beki Ales Mejac, wakihitaji kufanyiwa vipimo ili kujua kama watakuwa fiti kuweza kucheza mchezo huo.

Wakati huo huo, takwimu zinaoyesha kuwa timu ya Maribor imekuwa na matokeo mabaya dhidi ya timu za Kiingereza kwani katika michezo saba iliyocheza dhidi ya timu za Kiingereza imeshinda mchezo mmoja, imetoka sare mchezo mmoja na kufungwa michezo mitano.

Kikosi cha Maribor kinaweza kuwa hivi: Handanovic; Suler, Viler, Stojanovic, Filipovic; Viler, Mejac, Mertelj, Bohar; Ibraimi, Tavares

Timu ya Chelsea ambayo inaongoza kundi G ikiwa na alama saba baada ya kushinda michezo miwili na kutoka sare mchezo mmoja kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi ya mabingwa Ulaya wanaweza kuvuka hatua ya makundi ikiwa watashinda mchezo huo na kama Sporting Lisbon wakishindwa kuifunga Schalke 04 katika mchezo mwingine wa kundi G.

Chelsea inayofundishwa na kocha Jose Mourinho inatarajia kuendeleza rekodi yake ya kutokufungwa toka kuanza kwa msimu wa 2014/15 katika michuano mbalimbali huku mpaka sasa wakiwa wanaongoza kwenye msimamo wa ligi kuu nchini Uingereza

Timu ya Chelsea ambayo ni kwa mara ya kwanza inacheza nchini Slovenia inatarajiwa kumkosa mshambuliaji Loic Remy ambaye ni majeruhi hivyo kocha Jose Mourinho anaweza kumwanzisha Didier Drogba kuongoza safu ya ushambuliaji huku Diego Costa akianzia benchi kujiandaa na mchezo dhidi ya Liverpool pia nahodha John Terry anaweza kuanzia benchi kumpisha Kurt Zuma.

Kikosi cha Chelsea kinaweza kuwa hivi: Courtois; Luis, Zouma, Cahill, Ivanovic; Matic, Fabregas; Schurrle, Oscar, Hazard; Drogba

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!