Searching...
Image and video hosting by TinyPic
25 November 2014
Tuesday, November 25, 2014

Simba na Yanga bado wako usingizini!



 Na Samuel Samuel

Wakiamka wachezaji kama James Tungaraza " Bolizozo " , Saidi Nassoro "Mwamba" na Edward Chumila " Eddo Boy" katika usingizi wao wa milele na kutembelea mitaa ya Chamazi Complex na kujionea timu ambayo hawakuiacha katika ramani ya soka la nchi hii ilivyojiimarisha vizuri, watashikwa na butwaa! 

Lakini machozi yatawadondoka zaidi baada ya kuzitazama timu zao ambazo wameziacha zaidi ya muongo mmoja hakuna kilicho badilika , wataangua kilio. 

Wakati Azam FC, Kagera na Mtibwa Sugar zikijiinua kutokana na udhamini wa viwanda vyao achilia mbali udhamini mdogo toka kwa mdhamini wa ligi, Yanga na Simba zinajikongoja kupitia hisani za washika dau na udhamini "kichele" toka kwa wadhamini wao TBL.

 Lakini je, mapacha hao wanastahili kuishi maisha ya tabu kiasi hiki wakati ardhi waliyoikalia imejaa madini ?! Manchester United klabu inayosifika kuwa na uchumi mzuri zaidi duniani imejiinua kupitia madini ambayo Simba SC na Yanga SC wameyakalia tu. 

Man U mbali na udhamini kutoka katika makampuni mbali mbali, timu hiyo inayoshiriki ligi kuu nchini England imejiinua kupitia rasilimali watu ( madini haya) . 

Klabu hiyo ina mipango mizuri ya kujiimarisha kupitia wanachama na mashabiki wake. Je mashabiki wa Simba na Yanga wataishia kuzishangilia timu zao majukwaani tu? 

Kwanza kabisa klabu hizi zinatakiwa kuwa na mifuko ya maendeleo ya klabu. Simba ina matawi mangapi nchini? Yanga ina matawi mangapi? Kwa sera za vilabu hivyo , ili tawi lisajiliwe ni lazima liwe na wanachama hai wasiopungua 100. 

Kila kona kuna lundo la matawi haya swali ni je mbali na ada ya uanachama, kuishangilia timu jukwaani na kuzifuata timu zao popote zinapocheza mikoani kuna la ziada ? 

Uongozi wa vilabu hivi ni lazima vianzishe Mifuko ya maendeleo klabuni . Mifuko hiyo itachangiwa na matawi ili kuanza kutengeneza misingi ya uchumi inayotokana na klabu yenyewe 100% . 


Mathalani kila tawi nchini likapewa sharti la kukusanya sh 500,000 ambazo zitatokana na ada ya mwezi, klabu inaweza jikusanyia shilingi Milioni 10 kwa matawi 20 tu! na kwa mwaka ni sh 120 Milioni. Huu ni mfano tu. 

Hali hiyo pia itawajengea moyo wa kizalendo kwa wanachama nakujiona kweli ni sehemu ya mafanikio ya vilabu vyao. Mapato hayo ukichanganya na pesa za wadhamini, viingilio na washika dau klabu zitaanza kuiiona "Kanani" ya soka. 

Rasilimali watu kwa Yanga na Simba ni kama madini ambayo wameyakalia bila kujali thamani yake. Ni aibu mpaka leo klabu hazina viwanja vya kuchezea wala maduka ya kuuzia bidhaa zake. 

Amkeni jamani katika usingizi huo na kuzifanya klabu hizi zikue kiuchumi na kugeuka chachu ya maendeleo katika soka la nchi hii. Samuel Samuel -0652464525

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!