Searching...
Image and video hosting by TinyPic
5 November 2014
Wednesday, November 05, 2014

Nifikiliavyo mimi: Kina Brendan Rodgers wako wawili pale Liverpool


Na Chikoti Cico

Unaikumbuka Liverpool ya msimu wa 2013/14? unakumbuka magoli ya Luis Suarez? unakumbuka pasi ndefu na penati za Gerrard? unakumbuka kasi na chenga za Raheem Sterling na Coutinho? unakumbuka mchezo wa pasi fupi fupi wa Liverpool?

Unakumbuka nyimbo zilizoimbwa kwa hisia pale Anfield? Haya ni matukio machache kati ya mengi yaliyotokea kwenye msimu wa mwaka jana kwa timu ya Liverpool.

Ni ngumu kusahau hata kama ukitaka kujisahaulisha ila ukweli utabaki pale pale kuwa, Liverpool ya mwaka jana ilikuwa bora na ilitisha na kama sio matokeo mabaya ya mechi za mwisho kwenye ligi kuu nchini Uingereza, basi Liverpool ingeibuka bingwa mbele ya Manchester City na Chelsea.

Moja ya mechi iliyoonyesha ubora wa Liverpool kwa msimu uliopita ni mechi dhidi ya Arsenal ambayo iliisha kwa Liverpool kushinda kwa magoli 5-1 huku ndani ya dakika 20 tu za kipindi cha kwanza, tayari Liverpool walishafunga magoli manne kwenye huku wakicheza mpira wa kasi wenye nakshi za pasi fupi fupi.

Kuna mengi mazuri ya kuyazungumza kuhusu Liverpool kwa msimu uliopita ila kwa ufupi tu nyuma ya ubora wa timu hiyo kutoka Anfield kuna, maneno mawili tu ya kuyasema nayo ni “BRENDAN RODGERS”

Hakika huyu ndiye aliyeifanya Liverpool kumaliza ligi ikiwa imefunga magoli 101 huku mshambuliaji wake Luis Suarez akinyakua kiatu cha dhahabu baada ya kufunga magoli 31.

Brendan wa mwaka 2013/14 hakuwa mwoga kwenye kutafuta magoli na kutafuta ushindi, kwake msemo ulikuwa mmoja tu “The best way to defend is to attack” akimaanisha “njia nzuri ya kukaba/kuzuia ni kushambulia” na hakika alifanya hivyo kwa ubora wa hali ya juu na hatimaye akairejesha Liverpool kwenye michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya baada ya kuikosa kwa miaka mitano.


Huku mashabiki wa Liverpool wakiwa na shauku kubwa baada ya kurejea kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya, mfungaji wao hatari wa msimu uliopita Suarez akauzwa kwenda Barcelona na hapo ndipo Brendan mpya wa 2014/15 alipoanza kutofautiana na yule wa msimu wa 2013/14.

Katika kuziba pengo la Suarez Brendan akafanya usajili wa washambuliaji Rick Lambert na Mario Balotelli, usajili ambao mpaka sasa unaonekana kama ulikuwa wa pupa kwani hakuna kati ya washambuliaji hao ambaye ameonyesha kiwango bora mpaka sasa, huku Lambert akiwa sio chaguo la kwanza na Balotelli akiwa na magoli mawili tu kati ya mechi 10 za ligi.

Msimu uliopita Liverpool ya Brendan ilisifika kwa mchezo wa kasi ulionakshiwa na pasi fupi fupi, mchezo ambao uliimaliza Arsenal ndani ya dakika 20 lakini mpaka sasa wakiwa tayari wamecheza michezo 10 ya ligi na michezo minne ya ligi ya mabingwa Ulaya Liverpool, haionyeshi mchezo wowote wa kasi ama pasi fupi fupi.

Ni kama vile Brendan huyu sio yule wa msimu uliopita.
Msimu uliopita katika michezo 10 ya mwanzo ya ligi, Liverpool walishinda michezo saba na kutoka sare michezo miwili huku wakipoteza mchezo moja.

 Msimu huu kwenye michezo 10 ya mwanzo wa ligi kuu, Liverpool imeshinda michezo minne na kutoka sare michezo miwili huku ikifungwa michezo minne.

Mwisho kabisa Brendan Rodgers wa msimu huu, alifanya kitendo kilichoonekana kuwa cha dhihaka na aibu kwenye soka hasa kwenye ngazi ya ligi ya mabingwa wa Ulaya baada ya kuchezesha wachezaji wa akiba kwenye mchezo dhidi ya Real Madrid kitendo kilichowakera wapenda soka wengi duniani hasa ikizingatiwa kuwa ulikuwa ni moja ya mchezo ambao ulitarajiwa kuwasisimua wengi.

Wataalamu na wachambuzi mbalimbali wa soka duniani, wameita kitendo hicho kuwa ni cha aibu lakini pia ni tusi kwa timu kubwa na yenye historia kama Liverpool kukubali kuchezesha wachezaji wa akiba kwenye mechi kubwa kama hiyo huku sababu ikiwa kwamba mechi inayofuata ni dhidi ya Chelsea kwenye ligi kuu.

Labda ni mapema sana kuanza kuangalia tofauti ya Brendan Rodgers hawa wawili ila ukweli utabaki kuwa, Liverpool ya msimu huu bado haijaonyesha makali yoyote na bado jibu la nini kifanyike ili mambo yakae sawa Anfield ni maneno mawili tu ambayo ni “BRENDAN RODGERS”.

NAWASILISHA.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!