Searching...
Image and video hosting by TinyPic
2 November 2014
Sunday, November 02, 2014

Barcelona yachapwa 1-0 Camp Nou.


Na Oscar Oscar Jr

Barcelona wameendelea kusua sua kwenye ligi ya nchini Hispania baada ya kujikuta wakichezea kichapo mbele ya timu ya Celta Vigo ambayo kabla ya mchezo wa jana, ilikuwa inashika nafasi ya sita baada ya kujikusanyia alama 16. 

Celta Vigo wameonyesha hali ya kupambana msimu huu kwani mpaka sasa, wamepoteza mchezo mmoja pekee huku ushindi wao mbele ya Barcelona unakuwa wa tano msimu huu.

Kocha wa Barcelona, Luiz Enrique  ambaye msimu uliopita alikuwa kocha wa Celta Vigo, amejikuta akichezea kichapo cha pili mfululizo baada ya juma lililopita kufungwa na Real Madrid 3-1 kwenye mchezo wa El-Classico uliopigwa kwenye dimba la Santiago Bernabeu.

Huu ulikuwa mchezo wa kwanza wa nyumbani ambao ulimjumuisha mshambuliaji Luiz Suarez lakini, Barcelona hawakuweza kufurukuta licha ya mipira kutoka kwa Lionel Messi na Neymar Jr kugomba mwamba wa goli mara mbili. 

Celta Vigo hawakuwa na historia nzuri Camp Nou lakini, ubora wao umewafanya kupata ushindi kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1941. Celta Vigo wanaonekana pia kuwa na safu bora ya ulinzi ambapo mpaka sasa, wameruhusu mabao saba pekee.

Kocha Enrique amezungumza baada ya mchezo huo na kusema kuwa, wao wamesahau yaliyopita na kwa sasa, wanageukia kwenye mchezo wao wa Uefa dhidi ya Ajax Asterdam ambao utapigwa katikati mwa juma lijalo. 

Barcelona anashika nafasi ya pili kwenye kundi F la michuano ya klabu bingwa barani Ulaya baada ya kujikusanyia alama sita huku PSG, wakiongoza kundi hilo wakiwa na pointi saba.

Ushindi wa jana wa Real Madrid wa 4-0 dhidi ya Granada, unawafanya wafikishe pointi 24, alama mbili zaidi ya Barcelona na kuongoza ligi. 

Real Madrid imekuwa hatari msimu hasa kwenye safu ya ushambuliaji ambapo mpaka sasa wamefunga jumla ya magoli 25 na Christiano Ronaldo amefikisha mabao 17.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!