Searching...
Image and video hosting by TinyPic
6 September 2014
Saturday, September 06, 2014

Wenger na Welbeck, Van Gaal na utawala mpya Old Trafford.



  Na Chicoti (Cico cicod)
 0755 700 076


Dirisha la usajili barani Ulaya lilifikia tamati rasmi saa sita kamili usiku wa Jumatatu huku makocha wa timu mbalimbali wakikamilisha usajili wa wachezaji tofauti katika kuimarisha vikosi vyao. Katika ligi kuu ya Uingereza kocha Arsene Wenger alifanikiwa kumsajili Dany Welbeck kutoka Manchester United kwa ada ya paundi milioni 16. 

Baada ya kuumia kwa Giroud ambaye atakaa nje kwa miezi mitatu ilimlazimu Wenger kufanya usajili wa mshambuliaji mpya na hatimaye Welbeck akatua Emirates. 

Ukiangalia takwimu za magoli dhidi ya Welbeck ni ngumu kusema ni mshambuliaji hatari na ndiyo maana umekuwa ni usajili ambao unabezwa na kuonekana hautaleta manufaa kwa timu ya Arsenal lakini katika umri wa miaka 23 Welbeck yuko kwenye mikono ya kocha ambaye ni mtaalamu wa kukuza washambuliaji ambao walionekana ni wa kawaida na hatimaye kubadilika na kuwa washambuliaji mahiri kama ilivyokuwa kwa Henry , Weah na Bergkamp. 

Hivyo tutegemee mabadiliko chanya kwa Welbeck katika kuzifumania nyavu lakini pia timu ya Arsenal kufaidika na mshambuliaji mwenye uzoefu wa michuano mikubwa katika ngazi ya klabu tena katika umri wa miaka 23 huku akiwa bado ana hamu ya kushinda vikombe zaidi. 

Usajili wa Welbeck kutoka Manchester United kwenda Arsenal ukiuangalia kwa jicho la tatu unathibitisha utawala mpya wa kocha mpya wa United Luis Van Vaal, Welbeck zaidi ya kuwa mwingereza pia alikuwa mchezaji aliyeitambulisha timu ya Manchester United kwasababu ni mmoja wa wachezaji waliokulia kwenye mifumo na taratibu za Manchester. 

Mike Phelan kocha msaidizi katika kipindi cha Ferguson akihojiwa na vyombo mbalimbali vya habari alisema “Mtu kama Welbeck amekuwa sehemu ya utambulisho wa United na utambulishwo huo umevunjwa” akaendelea kusema “Kila jambo lina mwanzo wake na labda huu ni mwanzo wa jinsi mpya ya kufanya mambo kwa Manchester United na labda ndivyo soka linavyokwenda”. 

Maneno hayo ya Phelan yanakupa picha ya namna gani utawala wa kocha mpya Van Gaal unavyothibitishwa huku mfumo wa kukuza wachezaji vijana kupewa mgongo kwa sasa lakini pia kocha kukosa imani na wachezaji vijana na hili linaonekana wazi hasa baada ya wachezaji vijana kama Michael Keane, Nick Powell na Tom Lawrence kuuzwa ama kupelekwa kwa mkopo. 

Kuna msemo wa Kiingereza unaosema “The end justifies the means” ukimaanisha “Mwisho wa jambo huhalalisha njia iliyotumika” hivyo kwa njia ambayo anaitumia Van Gaal kuijenga Manchester United mpya kwa kufanya usajili wa wachezaji mbalimbali wa kigeni na kuupa mgongo mfumo wa ukuzaji vijana utasubiriwa kuona matokeo yake yatakuwa yapi ndani ya miaka mitatu ya mkataba wake ila ukweli utabaki kuwa kwasasa Manchester United inaendeshwa Ki Van Gaal.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!