Searching...
Image and video hosting by TinyPic
4 August 2014
Monday, August 04, 2014

Unaanzia wapi kumnyima mshahara Kipre Tchetche?



Na Oscar Oscar Jr

Wachezaji wengi ingawa sio wote wa kigeni wanaocheza kwenye ligi kuu ya Tanzania bara hususani wale wenye uwezo dimbani, wamekuwa wasumbufu sana. 

Ni jambo la kawaida kabisa kusikia wamerudi kwao pasipo uongozi wa vilabu vyao kuwa na taarifa, ni jambo la kawaida kabisa kuona wakichelewa kujiunga na kambi za klabu zao bila kuwepo taarifa yoyote rasmi na kwa sababu viongozi wengi wa klabu zetu wanawachekea, wala hawana wasiwasi!

Unapomchunguza mchezaji wa timu ya Azam Kipre Tchetche raia wa Ivory Coast, unagundua kabisa habari tofauti. Yuko kwenye ubora wake tangu ajiunge na wana lamba lamba hao, mfungaji bora wa ligi kuu msimu wa 2012/2013, mchezaji bora wa ligi kuu msimu uliopita wa 2o13/2014  lakini huwezi kumuona akifanya jambo lolote la utovu wa nidhamu.

Tchetche ni moja kati ya wachezaji wachache sana wa kigeni wanaojua kutimiza majukumu yao. Pamoja na kuwa kwenye orodha ya wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa ligi kuu, bado haonekani kujivuna wala sio mtu wa vyombo vya habari. 
Anapiga pesa ndefu mwisho wa mwezi na uwanjani anapiga mabao. Unaanzia wapi kumnyima Tchetche mshahara wake?

Kwenye dirisha hili la usajili Tchetche amehusishwa mara kadhaa kujiunga na klabu mbili kubwa za Simba na Yanga, timu ambazo huwachanganya wachezaji wetu wengi tu lakini kwake haikuwa habari kubwa. 

Ameendelea kuwa kimya na mtulivu, mwisho wa mwezi anapiga pesa na uwanjani anapiga mabao. Unaanzia wapi kumnyima mshahara Kipre Tchetche?

Katika biashara ambazo timu ya Azam imewahi kufanya kwenye usajili wa wachezaji, kwa Tchetche walilenga hasa. Ni kweli kuna muda mchezaji anapungua ubora lakini Tchetche amekuwa muda wote akionyesha namna mchezaji wa kulipwa anavyotakiwa kuwajibika.

Ni mtu anayepigana dakika zote 90, hafungi magoli ili kesho ajiunge na Simba, hatimizi majukumu yake ili kesho awavutie mabosi wa Yanga. Siku zote anawaza kuimarisha kiwango chake na kuitumikia timu yake ya Azam. Unaanzia wapi kumnyima mshahara mtu kama Kipre Tchetche?

Ni vigumu kuwapata wachezaji wa aina ya Tchetche ndiyo maana hata pacha wake Kipre Balou bado huwezi mlinganisha na ndugu yake. 

Ni vema wachezaji wa kigeni wakaiga mfano wa Kipre Tchetche, ni lazima watumikie klabu zao  kwa ubora na uadilifu mkubwa, ni lazima waonyeshe thamani ya fedha wanazolipwa, ni lazima waache longolongo.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!