Searching...
Image and video hosting by TinyPic
1 April 2014
Tuesday, April 01, 2014

NIONAVYO MIMI:EPL BADO NI LIGI BORA ULAYA





Na Oscar Oscar Jr
+255789784858
Rais Kikwete mwaka 2007 aliweza kufanya kitendo cha kishujaa na kuonyesha mfano pale alipojitoa na kwenda kupima virusi vya Ukimwi ili kuweza kujua hali yake na kuwa tayari kupewa huduma zinazopaswa endapo angekutwa na maambukizi ya virusi hivyo.Mungu jalia,Rais wetu alikutwa yuko salama,yeye na mkewe mama salma.Kutokana na tukio hilo,misemo mbalimbali ilianza kujirudia na hata mipya kuzaliwa.Unaringa, umepima? unajipitisha,unavigezo mama? ni baadhi tu ya misemo hiyo.

Kuna muda unakutana na mdada ambaye,nyuma hakuchezi wala mbele,hakutikisiki lakini anakwambia,anataka kushiriki mashindano ya Ulimbwende! Unavigezo dada? Umepima? wakati mwingine ni jambo la kawaida tu kukutana na "kijeba" aliyekomaa vigimbi vya miguu,naye anakueleza kuwa,ndoto zake ni kuja kumfunika mtanzania anayecheza kikapu huko Marekani,Hasheem Thabeet.Ukimtazama kijeba huyo,urefu wake ni kama wachekeshaji Aki na Ukwa kutoka nchini Nigeria! Unavigezo bro? unahoja? unamashiko?

Kuna mada ambazo ni vigumu sana kuzizungumzia na pindi zinapoanzishwa,mjadala wake,huwa hauishi.Ni kipi kilitangulia kati ya Kuku na Yai? nani zaidi kati ya Christiano Ronaldo na Lionel Messi? nani anastahili tuzo ya mwanasoka bora wa EPL msimu huu,kati ya Eden Hazard,Luiz Suarez na Yaya Toure?.Kinachosababisha ugumu au urahisi wa maswali niliyouliza hapo juu,ni vigezo vinavyotumika.Unavigezo? Umepima?

hiki ndicho nilichokusudia leo kuonyesha kuwa ligi ya EPL bado ndiyo ligi bora Ulaya licha ya changamoto na mapungufu yanayojidhihirisha siku za hivi karibuni. Unapoamua kuanzisha mjadala kama huu,ni lazima uwe jasiri na shujaa kama Rais Kikwete alipoamua kwenda kupima,kupokea majibu na kukubali kuyatangaza.Ulaya kuna ligi 5 bora na katika kuzibainisha,kila mmoja anaweza kutumia vigezo vyake.Kuna ligi ya La Liga(Hispania),Ligi 1 (Ufaransa),Bundesliga (Ujerumani),Seria A (Italia) na Barclays (Uingereza).

Mpaka sasa,Bayern Munich kutoka Ujerumani wameshatangazwa kuwa mabingwa wapya wa Bundesliga zikiwa zimesalia mechi 7 kumalizika kwa msimu.Juventus kutoka nchini Italia nao wanaongoza kwa tofauti ya alama 11 na hii ni baada ya kupokea kichapo cha hivi karibuni toka kwa timu ya Napol.Ufaransa,tayari PSG wanaongoza kwa tofauti ya alama 13 lakini,Uingereza na Hispania,mpaka sasa,hakuna anayeweza kujua ni nani ataibuka bingwa kati ya timu 3 za juu kwenye msimamo wa ligi hizo.Kwa kigezo hiki,La Liga na Barclays,ndiyo bora kwa sasa.

Pamoja na kuwa soka ni burudani,wenzetu wamejikita zaidi katika kutengeneza pesa nyingi sana kupitia mchezo huu.Katika takwimu za hivi karibuni,Real Madrid ndiyo timu tajiri huku ikifuatiwa na wapinzania woa Barcelona kwenye nafasi ya 2 na Bayern Munich,wakishika nafasi ya 3.Katika timu 10 tajiri duniani,Hispania wana timu 2,Ujerumani 1,Ufaransa 1,Uturuki ina timu 2 huku Uingereza ikiwa na timu 4 ambazo ni Man United,Man City,Arsenal na Chelsea.Kwa kutumia kigezo hiki,bado naiona ligi ya EPL ni bora Ulaya.

Nchini Hispania wiki iliyopita kulikuwa na mechi ya watani wa jadi kati ya Espanyol na Barcelona,lakini hakuna aliyejali.Mechi ya watani wa jadi nchini Ujerumani kati ya Borussia Dortmund na Schalke O4,maarufu kama Ruhr Derby,hukuna mtu anayetenga muda wake kuitazama,siku hizi hata mechi ya Inter Millan na Ac Millan kule Italia,watu wanazipotezea tu! Lakini,unapozungumzia mechi za watani wa jadi Uingereza Arsenal vs Spurs,Everton vs Liverpool,Man U vs Man City na nyingine nyingi,dunia nzima hutega masikio kutaka kujua,nini kimetokea baada ya dakika 90.Bado kwa kutazama kigezo hiki,naendelea kuamini kuwa,EPL ndiyo baba lao.

Mashabiki ndiyo nguzo katika mchezo wa soka na bila wao,utamu wa mchezo huo unapungua.Katika kuangalia timu zenye mashabiki wengi duniani,bado timu za Uingereza zimeendelea kutamba.Man United wakiendelea kuwa kileleni huku wakifuatiwa na Barcelona nafasi ya 2 na Madrid,wakishika namba 3.Timu nyingine zinazopatikana kwenye 10 bora ni Chelsea,Arsenal na Liverpool.Uingereza wana wakilishwa na timu 4,Hispania 2,Italia 3 na Ujerumani 1.Huu nao ni msumari wa moto wa EPL dhidi ya timu nyingine Ulaya.

Makocha nao wananafasi kubwa katika kuongeza ubora wa mchezo huu na katika Orodha ya makocha 10 wanaolipwa vizuri duniani,wa kwanza ni Pep Gaudiola (Bayern Munich),wa pili ni Jose Mourinho (Chelsea) na wa tatu,ni Marcello Lippi (Gaungzhou).Katika orodha hiyo,makocha kutoka EPL bado wameendelea kuwafunika wenzao ambapo,yumo kocha Arsene Wenger(Arsenal),David Moyes (Man United) na Manuel Pellegrin (Man City) ndiyo maana unaona narudia maswali yangu.unaringa,umepima? Unavigezo mbaba? kupitia hili,ukweli unaendelea kujidhihirisha.

Ni ukweli uliowazi kuwa,timu 2 kutoka Hispania(Real Madrid,Barcelona),zimekuwa kwenye ubora wa hali ya juu kwa muda mrefu,lakini timu nyingine 18 zilizosalia kwenye La Liga,hakuna kitu.Lakini,ndani ya misimu ya hivi karibuni,angalau,Atletico Madrid wamekuja na kuleta upinzani wa kweli.Mechi kubwa Hispani ni 2 tu msimu mzima ambapo,moja huchezwa Estadio Santiago Bernabeu na ya pili,hupigwa pale Nou Camp.Hizi ndiyo mechi ambazo hata ukiambiwa kuwa itachezwa saa 9 usiku,unaweza kusubiri ili ushuhudie burudani.

Olympique de Marseille na Olympique lyonnais,siku za nyuma walikuwa washindani wa kweli ndani na nje ya ligi kuu nchini Ufaransa,lakini ujio wa kina "bwana mapesa" PSG na msimu huu,As Monaco,nako kumekuwa hakuna jipya.Tumeshuhudia timu ya Olympique de Marseille kwenye ligi ya mabingwa ikitolewa hatau ya makundi huku ikigawa alama 3 nyumbani na ugenini kama hawana akili nzuri! Paris Saint German ndiyo timu pekee yenye nguvu na hao wengine,wote wanasua sua.

Bayern Munich ni wazi kuwa,wamekamilika kwenye kila kitu.Kutwaa mataji 3 msimu uliopita likiwemo la ligi ya mabingwa Ulaya na kutwaa bundesliga msimu huu huku zikiwa zimesalia takribani mechi 7 msimu kumalizika,bila kupoteza mchezo wowote ni ishara tosha kwamba,mabwana wameenea.Lakini,tatizo la ujerumani siwezi kulitofautisha na lile la Hispania.Mpinzani pekee wa Bavarians ni Dortmund na msimu huu,Borussia Dortmund hawakuwa vizuri na ndiyo maana imekuwa rahisi sana kwa Pep Gaudiola kunyakuwa taji mapema.Wachezaji wa Schalke 04,Bayern Liverkusen na wale wa timu nyingine,wote wanawaza kununuliwa na Bayern Munich na kuziacha timu nyingine 18 zikiwa dhaifu kwenye ligi hiyo.

Kitu pekee ninachokubali ni kwamba,,klabu za Barcelona,Real Madrid na Bayern Munich ni bora kwa sasa kuliko timu yoyote kutoka ligi kuu ya Uingereza,lakini ukizungumzia ubora wa timu zote 20 zinazoshiriki ligi kuu ,bado shilingi yangu naiweka EPL kuwa ndiyo ligi bora Ulaya.

Kuna imani kuwa EPL inatangazwa sana ndiyo maaana inawatu wengi.Jambo hili linaweza kuwa kweli au isiwe kweli kwa sababu,hakuna ligi Ulaya ambayo haitangazwi.kama Lionel Messi na Christiano Ronaldo wangekuwa wanacheza kwenye timu tofauti za EPL na sio La Liga,kuna uwezekano mkubwa sana,EPL ingezifunika ligi nyingine karibu kwenye kila kitu.

Kama nilivyosema hapo awali,mada kama hizi huwa zikianzishwa,hazimaliziki.Ngoja niishie hapa,naomba kutoa hoja. Nakaribisha mjadala,hivyo kama unachochote,unaweza kunitafuta kwenye ukurasa wangu wa facebook kwa jina la Oscar Oscar Jr au whatsapp kwa namba +255789784858.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!