Searching...
Image and video hosting by TinyPic
1 April 2014
Tuesday, April 01, 2014

GIGGS:UNITED SIO WANYONGE MBELE YA BAYERN



Mabingwa watetezi Bayern Munich wanapigiwa upatu kushinda lakini Manchester United hawajichukulii kuwa wanyonge timu hizo zitakapokutana kwenye mechi ya kwanza ya robofainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya uwanjani Old Trafford Jumanne, kwa mujibu wa Ryan Giggs. 

Kukutana kwa klabu hizo mbili kuu Ulaya kutafufua kumbukumbu za fainali ya ligi ya Klabu Bingwa Ulaya 1999 iliyochezewa Barcelona ambapo United walifunga mabao mawili dakika za mwisho na kuwalaza Wajerumani hao 2-1. 

Bayern walishinda kwenye safari yao ya majuzi zaidi pale jijini Manchester,walipolaza City 3-1 kwenye mechi ya makundi Oktoba na endapo leo watapata ushindi kama huo,bila shaka utahakikishia vijana hao wa Pep Guardiola kufuzu kwa nusufainali. 

Lakini Giggs, aliyecheza kwenye fainali hiyo miaka 15 iliyopita, anabaki na imani kwamba United wanaweza kuzima wapinzani hao ambao walishinda taji la Bundesliga wiki iliyopita. 

"Bila shaka Bayern ni timu kali," alisema Giggs, ambaye atakuwa na mechi moja tu nyuma ya rekodi ya Raul ya kucheza mechi 142 za Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kama atacheza Jumanne. 

Raia huyo wa Wales mwenye miaka 40 na ambaye sasa ni mchezaji kocha Old Trafford, aliambia wanahabari kwamba: “Ndio mabingwa watetezi na Pep Guardiola ameongeza wachezaji wengine wapya na ni timu kali sana. 

“Bila shaka wanapigiwa upatu na watu wengi lakini sisi ni Manchester United na tutakuwa Old Trafford na tumeshuhudia jioni nyingi za kukumbukwa, hasa Ulaya. 

“Kwa hivyo kama wachezaji, hatujichukulii kama wanyonge, tunajiona kama Manchester United ikicheza nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa. 

“Tunasubiri kwa hamu sana. Kuna mechi ambazo kama mchezaji hutaka sasa kushiriki. Tutaenda huko, na bila shaka itakuwa mechi ngumu lakini tuna imani.”

Ingawa wamepitia msimu mgumu wa kwanza chini ya David Moyes na wako nambari saba kwenye Ligi ya Premia, United wameshinda mechi zao zote nne nyumbani za Ligi ya Mabingwa. 

Moyes alikariri matumaini hayo ya Giggs, ingawa beki wa kushoto mwenye uzoefu mwingi Patrice Evra amesimamishwa kucheza mechi hiyo na atakosa fursa ya kufufua uhasama wake na Arjen Robben wa Bayern. 

"Tunajua kwamba siku yetu huwa nzuri kama timu nyingine yoyote ile lakini ni lazima tuonyeshe hayo mara nyingi,” Moyes alisema.
“Nina imani kwenye wachezaji na nimesema kutoka siku ya kwanza nikiwa hapa – hilo halijabadilika. 

“Ninahisi kwamba wachezaji wote wanataka kucheza, na naweza kuona hilo kutoka kwa mtazamo wao kwenye mazoezi. Wote wanataka kucheza mechi kubwa na hilo ndilo wachezaji hapa wamekuwa wakitaka miaka mingi.” 

Moyes atakuwa pia bila Robin van Persie aliyejeruhiwa huku  mabeki wa pembeni Rafael na Alex Buttner wakitiliwa shaka pia. Madifenda Rio Ferdinand, Chris Smalling na Jonny Evans wote walifanya mazoezi Jumanne. 

“Tuna shida safu ya ulinzi, bila shaka,” Moyes aliongeza.
“Lakini sitataja timu yangu leo, bila shaka si kwa Bayern na si kwenu (wanahabari), lakini tutafanya badiliko moja au mawili.”

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!