Searching...
Image and video hosting by TinyPic
22 March 2014
Saturday, March 22, 2014

YANGA YAMPIGILIA MSUMARI WA MOTO RHINO RANGERS 3-0



Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara timu ya Young Africans leo imeibuka na ushindi na mabao 3 - 0 dhidi ya wenyeji timu ya Rhino Rangers katika mchezo uliofanyika jioni ya leo katika dimba la Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Young Africans ambayo inapigana kuhakikisha inatete Ubingwa wake kwa mara ya pili mfululizo, iliingia uwanjani kwa lengo la kusaka pointi 3 muhimu jambo ambalo wamefanikiwa na kusogea nyuma ya Azam FC kwa tofauti ya pointi moja tu.

Ikiwatumia washambuliaji wake Saimon Msuva, Mrisho Ngasa, Jerson Tegete na Emmanue Okwi safu ya ushambuliaji ya timu ya Young Africans ilikosa mabao kadhaa ya wazi dakika 20 za mwanzo kutokana na ubovu wa uwanja.

Dakika ya 29 ya mchezo Jerson Tegete aliipatia Young Africans bao la kwanza baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa timu ya Rhino Ragers kufuatia mpira uliopigwa na Saimon Msuva kuokolewa na walinzi wa Rhino kabla ya kumkuta Tegete aliyeukwamisha mpira wavuni.

Timu zote ziliendelea kucheza kwa lengo la kusaka mabao kabla ya mapumziko, lakini mpaka dakika 45 za mchezo zinamalizika, Rhino Rangers 0 - 1 Young Africans.

Kipindi cha pili Young Africans waliuanza mchezo kwa kasi na dakika ya 68 ya mchezo mlinzi wa Rhino Rangers Laban Kambole alijifunga wakati akitaka kuokoa mpira wa krosi iliyopigwa na Saimon Msuva na kuifanya timu ya Young Africans kuhesabu bao la pili.

Hussein Javu aliyeingia kuchukua nafasi ya Jerson Tegete aliwaiunua mashabiki wa Young Africans dakika ya 90 ya mchezo kufuatia kuitumia vizuri pasi ya Emmanuel Okwi aliyewatoka walinzi wa Rhino na kumpasia Jvu aliyeukwamisha mpira wavuni.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamazika, Rhino Rangers 0 - 3 Young Africans.

Baada ya mchezo wa leo Young Africans inafikisha pointi 43 ikiwa katika nafasi ya pili nyuma ya Azam Fc yenye ponti 44 huku timu zote kwa sasa zikiwa zimecheza michezo 20 na kubakisha michezo sita kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom.

Young Africans: 1. Juma Kaseja, 2. Juma Abdul, 3.Oscar Joshua, 4. Nadir Haroub "Cannavaro", 5. Kelvin Yondani, 6. Frank Domayo, 7. Saimon Msuva, 8. Hassan Dilunga, 9. Jerson Tegete/Hussein Javua, 10. Mrisho Ngasa, 11. Emmanuel Okwi 

taarifa hii ni kwa mujibu wa website ya YANGA.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!