Searching...
Image and video hosting by TinyPic
28 December 2014
Sunday, December 28, 2014

Uchambuzi: Southampton vs Chelsea


Na Chikoti Cico

St Mary’s nyumbani kwa Southampton patawaka moto Jumapili hii ambapo timu hiyo itaikaribisha Chelsea kwenye mfululizo wa ratiba ya mechi za ligi kuu nchini Uingereza kipindi hiki cha sikukuu.

Southampton ambayo inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi huku ikiwa na alama 32 baada ya kunyakua alama tatu dhidi ya Crystal Palace wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo kwa nguvu ili kutafuta ushindi na kuendelea kujikita “top four”.

Kocha wa Southampton Mdachi Ronald Koeman kuelekea mchezo atawakosa Jay Rodriguez, Sam Gallagher na Jack Cork ambao ni majeruhi.

Pia beki wa kulia wa timu hiyo Ryan Bertrand atakuwa nje kwakuwa yuko kwa mkopo kwenye timu hiyo akitokea Chelsea na hawezi kucheza dhidi ya timu yake mama.

Kuelekea mchezo huo timu ya Southampton inaonekana kuwa na rekodi mbaya dhidi ya Chelsea kwani katika michezo 10 iliyopita ya ligi dhidi yao imeshinda mchezo mmoja huku ikifungwa michezo sita na kutoka sare michezo mitatu.

Pia takwimu zinaonyesha katika michezo tisa Southampton waliyocheza nyumbani St Mary’s rekodi zinaonyesha wamezuia nyavu zao kutikiswa mara sita yani “6 clean sheets” wakati huo huo mshambuliaji wa timu hiyo Graziano Pelle amefunga magoli saba katika mechi nane alizocheza kwenye uwanja wa St Mary’s

Kikosi cha Southampton kinaweza kuwa hivi: Forster; Clyne, Fonte, Alderweireld, Yoshida, Targett; Schneiderlin, Wanyama, Davis; Mane, Pelle

Kwa upande wa vinara wa ligi hiyo timu ya Chelsea ambayo inaongoza ligi ikiwa na alama 45 huku ikifuatiwa kwa karibu na timu ya Manchester City ambao wanashika nafasi ya pili wakiwa na alama 42, wanatarajia kuendeleza wimbi lao la ushindi na kuzidi kujikita kileleni mwa ligi hiyo.

Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho anaingia kwenye mchezo huo huku akiwa hana wachezaji ambao ni majeruhi hivyo anatarajiwa kufanya mabadiliko machache katika mchezo huo wa pili ndani ya siku tatu baada ya kucheza siku ya Ijumaa dhidi ya West Ham na kushinda kwa magoli 2-0.

Chelsea kuelekea mchezo huo wanaonekana kuwa na rekodi nzuri ugenini kwani katika michezo 12 iliyopita waliyocheza kwenye ligi wameshinda michezo minane huku wakifungwa mchezo mmoja na kutoka sare michezo mitatu.

Kikosi cha Chelsea kinaweza kuwa hivi: Courtois; Ivanovic, Terry, Cahill, Azpilicueta; Matic, Mikel; Hazard, Fabregas, Ramires; Costa

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!