Searching...
Image and video hosting by TinyPic
20 March 2014
Thursday, March 20, 2014

ARSENE WENGER NA MOURINHO USO KWA USO.Arsene Wenger ana nafasi ya kumnyamazisha Jose Mourinho Jumamosi timu yake ya Arsenal itakapozuru Stamford Bridge ikilenga kupokonya Chelsea uongozi wa kinyang’anyiro cha kushinda Ligi ya Premia.
Hakuna njia bora zaidi ya kusherehekea mechi ya 1 000 kwa kocha Arsene Wenger akiwa kwenye usukani  wa Arsenal kama kushinda na kuvunja rekodi ya kutofungwa nyumbani inayoshikiliwa na mdosi Jose Mourinho ambaye mwezi uliopita alipuuza mbali na kumtaja kuwa “mtaalamu wa kufeli”
.
Vita ya maneno imekuwa ikiendelea kwenye mbio za ligi ya premia lakini ni uwanjani ambapo alama hushindwa na kupotezwa. Matokeo ya dabi hiyo ya Jumamosi huenda yakawa na umuhimu mkubwa kuamua nani atakwua mshindi Mei 11. 

Chelsea walionekana kudhibiti vyema mbio hizo hadi wikendi iliyopita waliposhindwa 1-0 na Aston Villa. Ushindi wa Liverpool, Arsenal na Manchester City ulifanya mambo kuwa magumu zaidi kuelekea mbio za ubingwa. 

Timu hiyo ya Mourinho bado ina uongozi wa alama nne mbele ya Arsenal na Liverpool, ingawa wote wawili wana mechi moja ambayo hawajacheza, huku City walio alama sita nyuma ya Chelsea wakiwa na mechi tatu za kucheza. 

City watakuwa nyumbani kukabiliana na klabu ya Fulham inayoshika mkia kwenye ligi Jumamosi huku Liverpool wakisaka ushindi wao wa sita mfululizo ugenini kwa Cardiff City ambao wanapigana kukwepa shoka la kushushwa daraja. 

Wenger alitaja matamshi ya Mourinho kuwa ya “kijinga” na ya “kukosa heshima” mwezi jana baada ya kocha huyo Mreno kufanyia mzaha ukame wa mataji wa misimu minane wa Mfaransa huyo.
"Ninaogopa kufeli? Yeye ni mtaalamu katika kufeli. Mimi hapana. Kwa hivyo mtu akidhani kwamba hajakosea, na kwamba naogopa kushindwa, ni kwa sababu huwa sishindwi mara nyingi,” akasema Mourinho. 

Wenger alikuwa ameanzisha majibizano hayo alipouliza maswali kuhusu nia ya Mourinho kusema timu yake ni “farasi mdogo” kwenye mbio dhidi ya Manchester City ambao ni "jaguar".
Arsenal walionekana kuteleza baada ya kushindwa mara mbili mfululizo kwenye ligi, lakini ushindi wa 1-0 dhidi ya wapinzani wao kutoka London kaskazini Tottenham Hotspur wikendi iliyopita ulifufua matumaini yao ya kushinda taji hilo mara ya kwanza tangu 2004 – mwaka ambao Mourinho alifika mara ya kwanza London akijiita “the Special One” yaani Yule Mteule. 

Ushindi Stamford Bridge, ambapo Mourinho hajawahi kupoteza mechi ya ligi, utawaweka alama moja kutoka kileleni wakiwa na mechi moja ambayo hawajacheza, jambo ambalo litakuwa kibarua ikizingatiwa kwamba Jack Wilshere, Aaron Ramsey, Theo Walcott na Mesut Ozil wanauguza majeraha.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!