Searching...
Image and video hosting by TinyPic
3 July 2013
Wednesday, July 03, 2013

KELVINI YONDANI WA YANGA MCHEZAJI BORA VPL



BEKI wa Yanga SC, Kevin Patrick Yondan ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2013/2013 na kuzawadiwa donge nono la Sh. Milioni 5.

Hata hivyo, katika hafla ya kutoa zawadi za washindi wa Ligi Kuu msimu uliopita kutoa wadhamini, Vodacom Tanzania zilizofanyika katika hoteli ya Double Tree, Masaki, Dar es Salaam, usiku huu, Yondan hakuwepo na tuzo yake alipokelewa na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto, kutoka kwa mgeni rasmi, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara.

Yondan ambaye alikuwa katika msimu wake wa kwanza Yanga SC, yuko kwenye kambi ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayojiandaa na mchezo dhidi ya Uganda Julai 13, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kipa chipukizi wa Tanzania Prisons FC ya Mbeya, David Burhan alishinda tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu na kupewa Sh. Milioni 5, wakati mfungaji bora, Kipre Herman Tchetche raia wa Ivory Coast  wa Azam FC alipewa Milioni 5 pia na Fully Maganga wa JKT Mgambo alipewa tuzo ya mchezaji mwenye nidhamu na kuzawadiwa Milioni 5.  

Kocha mpya wa Simba, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ ameshinda tuzo ya kocha bora kwa kazi nzuri aliyoifanya akiwa na Kagera Sugar msimu uliopita na kuzawadiwa Milioni 7.5 sawa na refa bora, Simon Mbelwa.
 
Yanga SC pamoja na kuzawadiwa Sh. Milioni 70 za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, waliongezewa Milioni 15 kwa kuwa timu yenye nidhamu zaidi kwenye ligi hiyo msimu uliopita, hivyo kuondoka na jumla ya kiasi cha Sh. Milioni 85.

Azam FC washindi wa pili kwa msimu wa pili mfululizo, walizawadiwa Sh. Milioni 35, Simba SC washindi wa tatu Milioni 25 na Kagera Sugar washindi wa nne walipewa Milioni 20.

Kwa upande wa zawadi za wachezaji wa timu za vijana za klabu za Ligi Kuu, Hamisi Saleh (JKT Ojoro), Abdulrahman Mussa (Ruvu Shooting), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Chande Magoja (Mgambo JKT), Tonny Kavishe (Mgambo JKT) na Rajab Zahir (Mtibwa Sugar), wote wamezawadiwa Sh. Milioni 1 kila mmoja.
Zawadi za wachezaji wa timu za vijana, walizozawadiwa kwa kuzichezea mechi nyingi timu zao za wakubwa katika Ligi Kuu, zimetoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Rajab Zahir amesaini Yanga SC na tayari amejiunga nayo.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!