Wachezaji wa Yanga wapewa muda wa mapumziko.
Na Oscar Oscar Jr
Baada ya timu ya Yanga kujikusanyia alama sita katika michezo miwili waliyoshuka dimbani Jiji Mbeya, hatimaye leo kikosi kimerejea jijini Da es Salaam tayari kwa maandalizi ya safari kuelekea nchini Botswana kuikabili timu ya BDF11 kwenye mchezo wa marudiano wa kombe la shirikisho.
Mchezo wa awali Yanga waliweza kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 na hivyo wako kwenye nafasi nzuri sana ya kufuzu kwa hatua inayofuata kwenye michuano hiyo ya Afrika.
Katika mechi za hivi karibuni, Yanga wameonekana kuimarika sana hasa katika safu yake ya ushambuliaji ambapo katika mechi zao mbili zilizopita wamefunga mabao sita.
Ushindi dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City, umewafanya mabingwa hao wa kihistoria kwenye ligi ya Tanzania kuongoza ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 31 huku wapinzani wao wa karibu kwenye mbio za ubingwa msimu huu timu ya Azam baada ya kutoka sare kwenye mechi mbili mfululizo, wamejikuta wakishika nafasi ya pili wakiwa na alama 27.
Kocha msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa ameiambia E-Sports ya EFM kuwa, wachezaji wote wamepewa mapumziko ya siku moja na kesho watakutana kwa ajili ya kufanya maandalizi ya safari yao kuelekea nchini Botswana ambapo wamepanga kuondoka keshokutwa.
0 comments:
Post a Comment