Mapinduzi Cup: Mtibwa Sugar vs Simba
Na Oscar Oscar Jr
Mapinduzi Cup huko visiwani Zanzibar inaanza kutimua vumbi siku ya leo huku wenyeji, timu ya JKU wakiumana na timu ya Mafunzo na baadaye, kutakuwa na mchezo baina ya Polis dhidi ya Shaba.
Mechi ambayo inatazamiwa kuteka hisia za walio wengi hasa huku Tanzania bara, ni ile itakayopigwa Usiku baina ya Simba dhidi ya Mtibwa Sugar.
Mtibwa Sugar ambao ni vinara wa ligi kuu Tanzania bara wakiwa na pointi 16, watashuka dimbani leo hii kuwavaa wekundu wa Msimbazi, Simba ambao wanashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi kuu kwenye mchezo wa kundi C kwenye michuano hiyo ya kumbukumbu ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika mwaka 1964.
Mtibwa Sugar wataingia kwenye mchezo huu kama timu inayopewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi hasa ukizingatia rekodi na ubora walioonyesha msimu huu.
Mtibwa ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja wa ligi na pia ndiyo timu yenye safu bora ya ushambuliaji mpaka sasa wakiwa na magoli 11 sambamba na timu ya Yanga huku katika safu ya ulinzi, wakiruhusu mabao machache (Manne).
Simba ambao wamekuwa kwenye sintofahamu dhidi ya benchi lao la ufundi kufuatia taarifa za kuondoshwa kwa kocha wao mkuu ingawa hazijathibitishwa rasmi, wametua visiwani humo huku wakiwa na wachezaji pungufu na pia bila la kocha wao mkuu Mzambia, Patrick Phiri.
Kisaikolojia, timu haiko vizuri ingawa inaundwa na wachezaji ambao wana uzoefu wa mashindano mbalimbali na wanajua namna ya kuendana na mazingira magumu.
Emmanuel Okwi ambaye ndiye kinara wa mabao kwa upande wa Simba na mchezaji wa kutegemewa, atayakosa mashindano hayo kutokana na kurudi kwao kuendelea na fungate baada ya kufunga Ndoa hivi karibuni.
Simba ni timu ambayo bado haina muendelezo wa mchezo mzuri na hata ukirejea kiwango kizuri walichokionyesha kwenye mechi yao ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga, sio walichokuwa nacho kwenye mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar ambapo walipoteza kwa bao 1-0.
Mechi ya mzunguko wa kwanza baina ya timu hizi, ilishuhudia dakika 90 zikimalizika huku timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1 lakini katika mchezo wa mwisho wa kirafiki ambao ulizikutanisha timu hizo kwenye uwanja wa Azam Complex, Simba walichezea kichapo cha bao 4-2.
0 comments:
Post a Comment