Searching...
Image and video hosting by TinyPic
5 December 2014
Friday, December 05, 2014

RUNGU LA MTANI JEMBE KUMWANGUKIA NANI?



Na Samuel Samuel 
 0652464525
 
Kampuni yoyote ile inayojiendesha kibiashara ni lazima iwe na mipango endelevu katika kuhakikisha inatafuta masoko zaidi ya bidhaa zake ili mwisho wa siku izidi kufana katika faida. 

Moja ya njia za kujitafutia faida zaidi ni ushawishi mzuri wa bidhaa zake kwa kutumia njia mbali mbali ikiwemo uwekezaji na udhamini kwa taasisi zenye mtaji mkubwa wa rasilimali watu. 

Yanga na Simba ni timu pekee nchini zenye mashabiki wengi zaidi kuliko timu yoyote ile. Inakisiwa kila timu ina mashabiki wasiopungua Milioni saba na kuendelea. 

Kampuni ya Tbl kupitia kinywaji chake cha bia ya Kilimanjaro kwa pamoja inatoa udhamini kwa vilabu hivyo vikongwe zaidi nchini . Mbali na udhamini huo, Tbl kama ilivyo ada kwa makampuni yanayojiendesha kibiashara , iliamua kuanzisha shindano la mtani jembe. 

Shindano hilo ambalo limehasisiwa mwaka jana na Simba SC kuibuka bingwa kwa kuilaza Yanga SC bao 1-0, limegeuka mtihani mkubwa kwa makocha wa timu hizo mbili. 

TBL wanavuna mamilioni ya shilingi kupitia shindano hilo kutokana na kura zinazopigwa na mashabiki wa timu hizo kabla ya pambano. 

Wakati meneja wa TBL akiandaa kicheko kwa faida, mmoja wa makocha timu hizo hukalia kuti kavu na mwisho wa siku kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza ajira yake kama ilivyotokea mwaka jana kwa kocha wa Yanga, Ernie Brandts.

Tarehe 13 mwezi huu, mahasimu hao wa soka nchini watakutana katika pambano hilo maarufu kama " mtani jembe". Simba inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa pambano lililopita. 

Hebu tuziangalie timu hizo mpaka sasa, je kuti kavu litamkuta Patrick Phiri au Mbrazil Maximo? Ukiziangalia timu zote kuna mabadiliko makubwa yamefanyika ukilinganisha na pambano lililopita hasa upande wa Simba SC. 

Simba iliivaa Yanga ikiwa na kocha Logaruc lakini sasa inakwenda kuivaa Yanga ikiwa na Phiri . Isiaka, Manyika jr , Maguli, Okwi na mchezaji mpya, Danny Sserunkuma wote hao ni wageni katika pambano hilo.


Yanga mbali na kocha Maximo, wengine ni Coutinho, Emerson, Seme ambaye alikuwa Prisons kwa mkopo mwaka jana wote watakuwa wageni kwenye pressure ya mechi hiyo. 

Timu hizi kwa mara ya mwisho zilikutana Octoba 18 huku Dar Young Africans ikipewa nafasi kubwa ya kuibuka kidedea kwenye mechi  ya ligi lakini mwisho wa siku mechi ilikwisha kwa sare tasa ya 0-0.

Safu ulinzi ya Simba iliyokuwa ikiundwa na vijana chipukizi kuibuka kidedea kwa sifa kedekede baada ya kuwazuia wachezaji mahiri kama Ngasa, Coutinho, Jaja na Haruna Niyonzima. 

Mechi ijayo itakuwa ngumu sana na haitabiriki mpaka sasa baada ya timu zote kufanya usajili wa maana na zinaonekana kulingana katika maandalizi. 

Huku Yanga ikifanikiwa kuinasa saini ya kiungo mahiri kutoka nchini Brazil, Emerson vivyo hivyo Simba SC imefanikiwa kumsajili mshambuliaji hatari toka nchini Uganda , Sserunkuma. 

Phiri anasifika kwa mfumo wa 4-4-2 akiruhusu kiungo mkabaji awe injini ya timu kwa kuanzisha mashambulizi ya kasi na kuipanga timu kukaba mianya yote. 

Mkude amabye ni kiungo mkabaji tegemeo wa timu hiyo anakwenda kucheza mechi hiyo huku mifuko yake ikiwa imetuna kutokana na kuandikisha kandarasi mpya ya 60M na kupewa gari aina grand mark II Verosa. 

Hapo ni kufa na kupona kuwadhihirishia mabosi wake hawakukosea kumpa thamani hiyo. Maximo ambaye yawezekana ni kocha fundi zaidi nchini wa kujilinda kuliko kushambulia je ataendelea na mfumo huo au atabadilika baada ya kumpata. 

Kiungo mchezeshaji mwenye nguvu na kasi nzuri ya kupandisha timu, Emerson anaweza kuziba kabisa pengo lililoachwa na Frank Domayo kama Maximo atatumia mfumo ambao utairuhusu timu ishambulie kupita pande zote . 

Kwa kipindi sasa toka Mbrazil huyo aipokee timu kwa kocha Hans Pluijm, amekuwa akitumia mifumo ambayo inaifanya timu hiyo ionekane inajilinda zaidi na kushambulia kwa kasi ndogo kupitia katikati. 

Maximo ili kuipunguza kasi fowardya Simba ambayo ujio wa Sserunkuma unatoa taswira ambavyoinaweza kugeuka tishio ni lazima ashambulie ilikuwanyima uhuru mabekiwa pembeni kuanzisha mashambulizi na mwisho wasiku ama Okwi, Sserunkuma, Maguli kuleta madhara kwenye lango lake. 

Yetu macho tunasubiri kuona rungu la mtani jembe litamgonga nani? Nani ataungana na meneja wa TBL kucheka? Na nani huenda akaelekea Mwalimu JK international airport tayari kurudi nyumbani?!

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!