Na Oscar Oscar Jr
Timu ya Azam hatimaye imekamilisha usajili wa beki wa kati kutoka nchini Ivory Coast, Serge Pascal Wawa baada ya hapo jana mchezaji huyo kufuzu vipimo vya afya. Beki huyo alikuwa anacheza kwenye klabu ya Al- Merrikh ya nchini Sudan na sasa amejiunga rasmi na mabingwa hao wa Tanzania bara.
Azam wanajiandaa kwa michuano ya klabu bingwa Afrika na bila shaka haya ni maandalizi kuelekea michuano hiyo. Kwa sasa Azam ni timu ambayo ina wachezaji wengi wa kucheza nafasi ya beki wa kati na ujio wa Wawa, utamuongezea uwanja mpana kocha Joseph Omog kuteua kikosi cha kwanza.
Azam kwa sasa, wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu baada ya kukusanya alama 13 kwenye mechi saba za ligi kuu msimu huu. Katika mechi hizo, wamejikuta wakipoteza michezo miwili huku wakitoka sare mara moja na kushinda mechi zao nne.
Kutokana na sheria za TFF kuhusu wachezaji wa kigeni kutozidi watano, Azam watalazimika kuachana na mchezaji wake wa kigeni mmoja ili kutoa fursa ya Pascal Wawa kupokelewa na TFF. Mchezaji Diarra kutoka Mali na Lionel Saint Preux wa Haiti, kuna uwezekano mmoja panga likampitia.
12 November 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment