Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na benki ya CRDB zimeunda kikosi kazi (task force) kwa ajili ya kushughulikia matumizi ya tiketi za elektroniki ambayo yalisimamishwa kutoka na changamoto mbalimbali zilizokuwa zimejitokeza.
TFF na CRDB zimefanya kikao cha pamoja jana (Machi 20 mwaka huu) kuhusu masuala ya tiketi za elektroniki na kukubaliana kuunda kikosi kazi hicho kwa ajili ya uboreshaji matumizi ya mfumo huo. Kikosi kazi hicho kitakuwa na wajumbe kutoka TFF na CRDB.
Kwa upande wa TFF wajumbe wake ni Mkurugenzi wa Sheria na Uanachama, Evodius Mtawala, Ofisa Habari na Mawasiliano, Boniface Wambura na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Silas Mwakibinga. Rais wa TFF, Jamal Malinzi ametoa shukrani za kipekee kwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Dr. Charles Kimei ambaye alihudhuria binafsi kwenye kikao akiongoza timu yake.
Malinzi amesema ni imani ya TFF kuwa mfumo wa tiketi za elektroniki ndiyo mkombozi wa ulinzi wa mapato milangoni, na anaamini kwa pamoja TFF na CRDB zitafanikisha matumizi hayo ya tiketi za elektroniki. YANGA, RHINO KUCHEZA TABORA VPL Yanga inaumana na Rhino Rangers katika moja kati ya mechi mbili za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zitakazochezwa wikiendi hii katika miji miwili tofauti.
Mechi hiyo itafanyika kesho (Machi 22 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora ambapo kiingilio kitakuwa sh. 5,000 kwa jukwaa kuu na sh. 3,000 mzunguko. Nayo JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa Mbeya City katika mechi itakayochezwa kesho Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Ligi hiyo itaendelea keshokutwa (Jumapili) kwa mechi nne ambapo Simba itacheza na Coastal Union katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Azam itaoneshana kazi na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Azam Complex. Mechi hizo mbili zitakuwa ‘live’ kupitia Azam Tv. Mechi nyingine za Jumapili ni Mgambo Shooting dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, wakati Ruvu Shooting na Ashanti United zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. Boniface Wambura Mgoyo Media and Communications Officer Tanzania Football Federation (TFF)
0 comments:
Post a Comment