Searching...
Image and video hosting by TinyPic
21 March 2014
Friday, March 21, 2014

INIESTA ADAI WATAWACHAKAZA REAL MADRID.



Kiungo mashuhuri wa Barcelona Andres Iniesta amewapa wenzake changamoto kwa kutangaza kuwa wana uwezo wa kukomesha uhafifu ugenini na kuwachakaza viongozi wa ligi ya La Liga, Real Madrid, katika kivumbi cha Jumapili kinacho ngojewa na wengi almarufu kama ‘El Clasico’ kitakacho anguka uwanja wa Bernabeu. 

Barca, ambao ni mabingwa watetezi, wanashikiria nafasi ya tatu baada ya kushinda mechi moja kati ya tano za mwisho ugenini na ikiwa watafaulu kuwalaza maadui wao wa jadi, watafunga mwanya kati yao hadi alama moja pekee.

Iniesta ametumia mfano wa ushindi wao dhidi ya wakwasi wa Uingereza, Manchester City, kwenye mkondo wa 16-bora katika shindano la Champions League, kama kigezo kuwa Barcelona wana uwezo wa kuwanyamazisha watanashari wao. 

“Tumekuwa na kipindi kibaya kama yeyote katika mchezo huu lakini si kumaanisha Madrid watatutawala rahisi. Ni vigumu kutafakari kuwa kuna mashabiki wa Barca ambao wamepoteza imani nasi.
“Tumedhihirisha kipawa chetu cha kugeuza matokeo mabaya liwalo liwe na kuwachapa Madrid ni njia moja ya kukumbusha kila mtu tunaweza,” Iniesta alisema katika kongamano la wanahabari. 

Mwalimu wake Gerardo Martino ana starehe ya kuchagua kutoka kikosi chake kamili na anatazamiwa kuwatumia viungo aliowashirikisha kwenye mechi ya mkondo wa pili dhidi ya City.
Nyota Neymar na Cesc Fabregas wanatazamiwa kurejea baada ya kupumzishwa katika ushindi wao wa kishindo wa 7-0 dhidi ya Osasuna juma lililopita huku Pedro Rodriguez na Alexis Sanchez waliokuwa miongoni mwa wafungaji wakiwapisha. 

“Ni lazima tucheze vyema zaidi kwani wapinzani wetu watadai hivyo na badala ya kuwaza kuwahusu, tunastahili kufikiria juu yetu. Tunastahili kuonyesha ujasiri,” Iniesta aliongeza.
Madrid hawajapoteza katika mechi 31 zilizofuata baada ya kunyukwa 2-1 na Barcelona pale fahari hawa walipokutana mara ya kwanza mapema kwenye msimu katika uwanja wa Nou Camp. 

Kufuatia kushamiri huko, vijana wa Carlo Ancelotti, wameweza kuwapiku Barca na Atletico Madrid na kuketi kitako katika uongozi wa La Liga huku wakifuzu fainali ya kombe la Copa Del Rey na robo fainali ya Champions League. 

“Tangu mechi ya kipindi cha kwanza katika msimu, tumeimarika sana lakini ni lazima tuwe katika kiwango cha juu zaidi ili kuwalaza Barca. Itakuwa mechi ngumu lakini hatuna budi ili kuwa katika asilimia 100 dhidi yao,” kocha Ancelotti alisema. 

Raia huyo wa Italia alipata pigo pale nyota chipukizi, Jese Rodriguez, alipoumia goti kwenye mechi yao ya marudiano dhidi ya Schalke Jumanne lakini ana zana kali za kutumia ili kutawala Jumapili.
Staa wake Luka Modric, Angel di Maria, Gareth Bale na Karim Benzema watarudi ulingoni baada ya kupumzishwa dhidi ya Schalke katika kivumbi kitakacho kutanisha mchezaji bora zaidi duniani, Ronaldo kwa upande wa Madrid na asimu wake aliyeshikilia taji hilo miaka minne mfururizo, Lionel Messi.

Ikiwa wawili hao watafanikiwa kutoshana nguvu, Atletico wanamiliki nafasi ya pili ndio wataweza kufaidika pakubwa kwani wanawatembelea Real Betis wanaovuta mkia kwenye ligi hiyo.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!