BENCHI la Ufundi la Azam FC limetamka kuwa
halitafanya usajili wowote wa mchezaji mpya kwa ajili ya msimu ujao,
badala yake litaanza programu ya kupandisha vijana kwenye timu hiyo
kupata uzoefu.
Kocha msaidizi wa timu hiyo, Kally Ongala
aliliambia Mwanaspoti juzi Alhamisi jijini Dar es Salaam kuwa umefika
wakati wa kuvuna kile walichokipanda.
“Hatuna matarajio ya kuongeza mchezaji mpya kwenye
usajili ujao. Badala yake tutaanzisha utaratibu wa kuwapandisha vijana
kutoka kwenye taasisi yetu, waweze kuonyesha uwezo wao na kukomaa
kimashindano.”
Kally alisena kuwa kuna baadhi ya wachezaji ambao
tayari walishawapandisha kwa lengo la kupata uzoefu kama kipa ambaye
ameitwa na Kocha Kim Poulsen kwenye timu ya Taifa Stars, Aishi Manula.
“Nafikiri umefika wakati muafaka wa kuwapandishwa
wengine na kuonyesha kile ambacho walikuwa wakijifunza tangu mwanzo na
kuisadia timu yao,” alisema Kally mchezaji wa zamani wa Yanga na
Kajumulo na Azam kabla ya kujikita katika kazi ya ukocha.
Alisema wanakiamini kikosi chao kuwa ni bora na
ndiyo maana wamepanga kutosajili mchezaji yeyote mpya katika dirisha la
uhamisho wa wachezaji litakapofunguliwa rasmi.
“Tulichokifanya ni kuboresha mikataba ya wachezaji
wetu iliyokuwa ikikaribia kumalizika na wale ambao walikuwa wakicheza
kwa mkopo kuwapa mikataba,” aliongeza.
Aliongeza kuwa wanaamini wana kikosi imara ambacho
kinaweza kukabiliana na timu yoyote na pia kufanya vizuri katika
mashindano ya Kombe la CAF mwakani na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Pia, alisema kuna baadhi ya wachezaji watatolewa
kwa mkopo kama ilivyokuwa kwa Mrisho Ngassa ingawa alikataa kuweka
majina yao hadharani.
Imefahamika kwa wachezaji Uhuru Suleiman aliyekuwa
akicheza kwa mkopo pamoja na kipa Deogratius Munishi . aliyesimamishwa
kwa tuhuma za kupokea rushwa wameachwa wakati Gaudence Mwaikimba na
Malika Ndeule wakitarajia kwenda kwa mkopo Ashanti United iliyorejea
Ligi Kuu Bara.
0 comments:
Post a Comment